AMEACHA gumzo. Pasi zenye macho, uwezo wa kukaba wa kiungo, Thabani Kamusoko ‘Rasta’ umemfanya beki wa kati na nahodha wa Cercle De Joachim, Mghana Nartey Isaac kudai Mzimbabwe huyo ndiye aliyeifanya timu yao ifungwe.
Isaac ambaye ni miongoni mwa wachezaji watatu wa kikosi hicho kutoka Ghana akiwamo kipa, Isaac Abraham na straika, Odane Abrahamu, alisema Kamusoko ndiye aliyeizima timu yao kwa kuwa kiunganisha kizuri katika kikosi cha Yanga.
“Yule jamaa mwenye rasta ndiye aliyekuwa kiunganishi kizuri cha wapinzani wetu, alijua kuunganisha timu na kuifanya icheze na hakutoa nafasi upande wao ushambuliwe kirahisi,” alisema.
Pia winga, Simon Msuva, alimrahisishia kazi Kamusokokwenda kulisha washambuliaji mbele.
“Nikimzungumzia mchezaji mmoja mmoja, yule rasta (Kamusoko) naweza kusema ndiye alikuwa kama injini yao. Nimempenda namna anavyounganisha timu yake, anajua apige wapi mpira ili ufike salama, anajua kukadiria kila kitu,”alisema Isaac.
“Na alishirikiana vizuri na yule namba 27 (Simon Msuva) mwenye mbio ikawa rahisi kwao, naweza kusema yule ndiyo ametuua, mpira anaujua haswa na hata mechi ijayo, inabidi tuwe makini naye.”
Kocha ajifariji
Baada ya tumaini la ushindi kutoweka, Kocha Mkuu wa Cercle de Joachim, Abdel Ben Kacem, alisema kuwa Yanga wameponea chupuchupu kwao na hawajakata tamaa kwa kuamini watakuja kushinda Tanzania katika mechi ya marudiano. Ben Kacem ambaye ni raia wa Morocco, aliyecheza soka kwa muda mrefu Ubelgiji, alisema walifanikiwa kuidhibiti Yanga, lakini hawakuwa na bahati ya kufunga mabao.
“Yanga ni timu nzuri sana, lakini sisi tumecheza vizuri isipokuwa tu bahati haikuwa yetu, wachezaji wangu wamepoteza nafasi nyingi za mabao ila tutaonana Tanzania.”
Akizungumzia ufundi Ben Kacem alisema, makosa waliyofanya wachezaji wake ni madogo tu kama kutokuwa umakini na hii inasababishwa na ugeni katika mashindano hayo makubwa.
Mwandishi aishangaa
Kumbe Yanga inafahamika Mauritius bwana. Mwandishi Mwandamizi wa Mauritius, Bouckpi Illay, alishindwa kuvumilia na kutoa dukuduku lake baada ya kuiona Yanga na kuhoji, kama aliyokuwa akiiona ni Yanga kweli au anaota.
Unajua kwa nini? Bouckpi (72) anayeifanya kazi ya uandishi wa habari kwa miaka 50 sasa, alisema amekuwa anaifuatilia Yanga kwa miaka mingi anajua ni timu nzuri yenye ushindani mkubwa Afrika, lakini ilivyocheza katika katika Uwanja wa New George ni kama walikuwa wanafanya mazoezi.
“Mimi ni mwandishi mkongwe sana, nina muda mwingi katika kazi hii na nimekuwa nikiifuatilia kwa muda mwingi Yanga hiki siyo kiwango chao, sijui wameizarau hii timu yaani ni kama wanafanya mazoezi,” alisema Bouckpi ambaye anaandikia gazeti la Le Maurician and Weekend.
Alisema, anachojua klabu yao ni kawaida tu kucheza kwa kiwango hicho kwao ni kama wamelala, lakini Yanga aliyoiona ni kama wanazuga.
Credit:Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment