
KOCHA wa Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm, amewapa maneno mazito wachezaji wake saa chache kabla ya kikosi cha timu hiyo kupanda ndege kuelekea nchini Mauritius kucheza mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya nchini humo.
Leo Yanga itashuka katika Uwanja wa George V uliopo katika mji wa Curpipe kuwavaa Cercle de Joachim ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa raundi ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.
Kabla ya mabingwa hao kukwea pipa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Pluijm amewataka wachezaji wa kikosi hicho kila mmoja kujitolea kwa nafasi yake uwanjani kuhakikisha wanaipa mafanikio timu hiyo.
“Kila mmoja wenu lazima acheze kwa kujitolea,” alisema Pluijm. “Mpira wa sasa umebadilika hakuna timu ya kudharau, kila mmoja wenu lazima aelewe hilo kama mnataka kupiga hatua kimaendeleo kutoka hapa mlipo.
“Hakuna mechi rahisi, kila mmoja wenu lazima ajitambue na mcheze kwa kujitolea, umakini na nidhamu ni vitu muhimu vya kuzingatia wakati mkiwa uwanjani mkitafuta ushindi kila mmoja awajibike awe na nidhamu ya mchezo.
Pluijm aliendelea kuwapa maneno hayo ya busara wachezaji wake kwa kuwaambia kuwa wanatakiwa kubadilika na kila mmoja wao atambue kuwa amepata nafasi ya kusafiri nje ya nchi na wanatakiwa kuheshimu kazi yao na kucheza soka kwa kujituma kama wanataka mafanikio ya soka.
“Kila mmoja wenu amepata nafasi ya kutoka nje ya nchi, lazima mjitambue tunaenda wapi na tunatakiwa kufanya nini lakini pia lazima muheshimu kazi yenu ya mpira kama mnataka kupiga hatua kubwa zaidi ya hapa mlipo,” alisema.
Mechi hiyo inatazamiwa kuanza saa 9.30 kwa saa za Mauritius sawa na saa 10.30 kwa saa za Tanzania, mechi itapigwa katika Uwanja wa George V ambao hutumiwa na klabu hiyo ya Cercle de Joachim wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 6,200.
Chanzo:Bingwa.
0 comments:
Post a Comment