KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amechekelea sare ya kutofungana kati ya Azam FC na Tanzania Prisons iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza na BINGWA jana jijini Dar es Salaam, Pluijm alisema sare hiyo inawaweka Azam FC katika wakati mgumu kutokana na upinzani mkali uliopo baina yao.
Azam FC ilihitaji kushinda mchezo wao wa kiporo ili irudi kileleni mwa Ligi Kuu Bara lakini matokeo ya mchezo wao juzi yanawafanya kukabana koo na Yanga wote wakiwa na pointi 46, lakini wakiwa wamezidiwa idadi ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Pluijm alisema matokeo waliyopata Azam FC yamezidi kuwaongezea (Yanga) ari na kasi zaidi kuelekea mbio zao za kutetea ubingwa Ligi Kuu Bara msimu huu licha ya kuwa mgumu ukilinganisha na msimu uliopita.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema atahakikisha wanashinda michezo yao miwili ili wazidi kubaki kileleni na hii ni baada ya Azam FC kushindwa kuondoka na pointi zote tatu katika mchezo wao wa juzi.
Yanga imepangwa kucheza na Mtibwa Sugar mchezo wao wa kiporo Machi 1 mwaka huu na siku nne baadaye kukipiga na Azam FC, michezo yote miwili ikichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Tunacheza na Mtibwa Sugar na Azam FC katika michezo yetu miwili ijayo ambayo yote ni migumu, lakini lazima tufanye kazi ya ziada kuhakikisha tushinda, hii itatupa mwanga zaidi katika harakati za kutetea ubingwa wetu kila kitu kinawezekana,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema Yanga ina kila sababu ya kutetea ubingwa wake msimu huu kutokana na ukweli kwamba, kikosi chake kimesheheni wachezaji nyota wenye vipaji.
Katika hatua nyingine, Pluijm alisema kikosi chake kilishindwa kupata mabao mengi katika mchezo wa Kombe la FA hatua ya 16 bora dhidi ya JKT Mlale uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na nyota wake kucheza kwa tahadhari kubwa.
“Tuna mchezo wa kimataifa Jumamosi (dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius) na wachezaji walicheza kwa tahadhari kubwa kuogopa kupata majeraha lakini kila kitu kipo sawa, tuna imani ya kuendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata,” alisema.
0 comments:
Post a Comment