
Juma Luizio ni striker wa kitanzania anayecheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Zesco United ya nchini Zambia ambayo inashiriki ligi kuu ya nchini humo.
Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Mkoani Morogoro anasema hajawahi kujuta wala hakuna kitu ambacho amekosa kutokana na kutocheza kwenye vilabu vikongwe nchini vya Simba na Yanga.
Luizio amesema siku zote malengo yake yalikuwa ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na amefanikiwa katika hilo japo bado anataka kuhakikisha anasonga mbele zaidi kwenda kwenye nchi za kisoka zaidi ya Zambia ambako yupo kwa sasa.
Sports Bar ya Clouds TV imefanya mahojiano na mchezaji huyo ambaye mara kadhaa ameitwa kwenye timu ya taifa lakini mara nyingi amekuwa akiachwa na yeye ametaja baadhi ya sababu za kutoitwa mara nyingi kwenye timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
Sports Bar: Wachezaji wengi wa Tanzania wamepita kwenye vilabu vya Simba na Yanga lakini wewe hujawahi kucheza kabisa kwenye vilabu hivyo vikongwe, unadhani umekosa nini kutocheza kwenye timu hizo?
Luizio: Kiukweli hakuna kitu ambacho nimekosa kutopitia timu hizo, kwasababu hata wazazi wangu walikuwa hawapendi nipite kwenye hizo timu mbili. Kwa mfano baba alikuwa anamfuta hadi bosi wa Mtibwa na kumwambia kama timu hizo zitatokea zinamuhitaji mtoto wangu naomba usimuuze.
Sports Bar: Unadhani kwanini babayako alikuwa hapendi wewe upite kwenye vilabu vya Simba na Yanga?
Luizio: Kwasababu alikuwa anaona wachezaji wengi wanaenda pale halafu wanaisha. Kwamfano Juma Javu, alipoona kaenda pale halafu wakawa wanamsumbua wakati alikuwa anauwezo halafu hapati nafasi ya kucheza ndiyomaana akawa ananizuia kwenda kujiunga na timu hizo ingawa wenyewe walikuwa wananisumbua wananihitaji.
Hata mimi mwenyewe sikuwa tayari, ndoto zangu zilikuwa ni kwenda nje kucheza mpira wa kulipwa ndiyo maana sikuwa na presha ya kwenda kwenye timu hizo.
Sports Bar: Kwanini hauitwi mara nyingi kucheza kwenye timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’?
Luizio: Kutokana na majeraha nilikuwa sichezi kwenye klabu yangu. Kwasababu hata kocha anaangalia wachezaji wanaocheza mara kwa mara kwenye klabu zao, lakini mimi mechi za mwishomwisho nilikuwa sichezi.
Sports Bar: Kuna mawasiliano yeyote kati yako na kocha au viongozi wa timu ya taifa?
Luizio: Sio kocha, ila kuna baadhi ya viongozi wa TFF walikuwa wananipigia simu nazungumza nao.
Sports Bar: Unamipango na malengo gani kwenye maisha yako ya soka, au ndiyo tayari umeshafika hapo Zesco United?
Luizio: Mipango yangu mikubwa ni kuondoka pale na kwenda kwenye nchi za kimpira zaidi.
Credit:http:shaffihdauda.co.tz
0 comments:
Post a Comment