BENCHI la Ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limefurahishwa na kiwango cha timu hiyo walichokionyesha katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mbeya City, uliofanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya siku ya Jumamosi.
Kiwango hicho bora kiliifanya Azam FC kupata ushindi wa pili mnono kwenye ligi msimu huu kwa mechi za ugenini baada ya kuichapa Mbeya City mabao 3-0, ushindi wa kwanza mkubwa ugenini ulikuwa dhidi ya JKT Ruvu (4-2), uliofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mabao ya Azam FC yalifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 41, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ (dakika ya 63) na Farid Mussa aliyeingia kipindi cha pili akishindilia msumari wa mwisho dakika ya 84.
Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa walionyesha kiwango safi baada ya kufanyia kazi udhaifu uliojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kushindwa kuutendea haki mfumo wa 3-5-2 wanaoutumia.
“Tulijitahidi kufanya mazoezi kuondoa kiwango cha chini haraka iwezekanavyo katika mfumo wetu na nadhani kiwango chetu kilikuwa cha hali ya juu. Tulianza kwa ari ya chini, tulionekana ari yetu ya kujiamini ilikuwa chini dakika 10 hadi 15 za kipindi cha kwanza na hii ilitokana na matokeo tuliyopata wiki iliyopita (Coastal Union).
“Lakini baada ya hapo tulianza kujenga vema kiwango chetu na nadhani kipindi cha pili tulikuwa vizuri zaidi, tulifanya mabadiliko ya kimbinu kipindi cha pili, tulimpeleka Messi (Ramadhan Singano) katikati na kumchezesha Farid (Mussa) upande wa kushoto aliyeingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya,” alisema.
Hall alisema walifanya mabadiliko ya kumtoa Mudathir ili kuiongezea ubora wa timu eneo la katikati baada ya kipindi cha kwanza kukosa mtu wa kuwaunganisha vema wachezaji na kubakia kucheza sana mipira mirefu.
“Messi alikuwa mzuri sana katikati na ndiye mchezaji wetu bora katika kipindi cha pili, tulicheza sana mipira mirefu kipindi cha kwanza na kukosa mtu wa kuwaunganisha wachezaji, alipoingia Messi katikati aliweza kutekeleza vizuri jambo hilo na kuanza kucheza mpira safi na nimefurahia hali sisi kutoruhusu bao kwani ni jambo zuri,” alisema.
Mwingereza huyo aliongeza kuwa siku zote hawaamini waamuzi na ndio jambo kubwa lililomfanya ampumzishe takribani dakika 25 za mwisho Nahodha Msaidizi Himid Mao na kuingia Frank Domayo, ikiwa ni baada ya kiungo huyo bora mkabaji kuonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza.
Mipango mechi vs Tanzania Prisons
Kocha huyo wa zamani wa Academy ya Birmingham City, Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, alisema wanataka kuendeleza ushindi walioupata jana kwa kuifunga Tanzania Prisons licha ya kukiri kuwa itakuwa ni mechi ngumu.
“Itakuwa mechi ngumu, na siku zote ni ngumu, unajua mechi ya nje siku zote ni ngumu, hivyo tunatakiwa kuendeleza ushindi, lakini kushinda 3-0 ugenini ni matokeo mazuri sana, tunatakiwa kubakia katika hali hiyo ya kujiamini hadi kwenye mchezo ujao,” alimalizia.
Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Jumatano Februari 24 kucheza na Tanzania Prisons katika mchezo wa kiporo, ambao unaweza kuipeleka kileleni kwenye msimamo endapo itawachapa maafande hao kwani watafikisha pointi 48 na kuzizidi kete Simba (45) na Yanga (46).
Matajiri hao wa Azam Complex pia watakuwa wamebakiwa na mchezo mmoja wa kiporo watakaocheza na Stand United Machi 16 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment