Baada ya kufanikiwa kuwafunga Simba, mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Amissi Tambwe, ametamba kuwa kufunga ndiyo kazi yake, hivyo ataendelea kufunga kila siku.
Mshambuliaji huyo raia wa Burundi, alifanikiwa kuifunga timu yake ya zamani ya Simba juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0.
Mrundi huyo, alitemwa na Simba kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita kwa kile kilichodaiwa uwezo wake umeshuka wakati timu hiyo ikinolewa na Mzambia, Patrick Phiri.
Tambwe alisema kuwa yeye kazi yake ni kufunga mabao pekee siyo kingine, hivyo ataendelea kupachika kila siku.
Tambwe alisema anaamini bado ana uwezo mkubwa wa kufunga na huyo mshambuliaji wa Simba Amissi Kiiza ajiandae kutoka juu kwenye orodha ya wafungaji bora.
Tambwe alisema haoni sababu ya kutompita Kiiza kwenye ufungaji bora kutokana na kubakiza kiporo cha mechi ya ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Simba walisitisha mkataba wangu kwa madai kuwa uwezo wangu wa kufunga umeisha sasa nataka kuwathibitishia kuwa mimi bado nipo fiti kwa kufunga mabao kila mechi.
“Kama nimewafunga wao wanaojisifia wana safu nzuri ya ulinzi na hawajapoteza mechi sita za ligi kuu, nini kitanishinda?
“Sasa ninawaambia kuwa, nikiamua jambo langu hakuna anayeweza kunizuia, kama nilivyoamua kuwafunga wao katika mechi hii,” alisema Tambwe.
Credit:Salehjembe
0 comments:
Post a Comment