Ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, umempa ulaji Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm anayeandaliwa mkataba mwingine wa miaka miwili kubaki kuendelea kukinoa kikosi hicho.
Mholanzi huyo, ameweka rekodi nzuri msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa kufanikiwa kuifunga Simba mara mbili nyumbani na ugenini.
Yanga wikiendi hii ilikamilisha rekodi hiyo ya kuifunga Simba msimu huu kwa kuwachapa wapinzani mabao 2-0 yakifungwa na Donald Ngoma na Amissi Tambwe mwenye mabao 15 katika orodha ya wafungaji bora.
Taarifa zinaeleza uongozi wa Yanga umeanza kufikiria suala la kuanza mazungumzo na kocha huyo kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kubaki Jangwani.
Uongozi na mabosi hao, kikubwa walichoshawishika kumuongezea mkataba mwingine kocha huyo ni utendaji wake mzuri wa kazi kwenye timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, pia rekodi nzuri ya msimu huu ya kuwafunga watani wao wa jadi mara mbili walizokutana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Bosi huyo aliongeza kuwa, kwa pamoja viongozi wote wamekubaliana na kumuongezea mkataba, hivyo hivi sasa wapo kwenye maboresho ya baadhi ya mahitaji yake kuhakikisha wanamuongezea huo mkataba mpya.
“Kwa rekodi hii aliyoiweka Pluijm kwa kuifunga Simba mara zote mbili tulizokutana katika ligi kuu, inatosha kabisa kamati ya utendaji kumuongezea mkataba mwingine.
“Hivi sasa uongozi upo kwenye mazungumzo na kocha huyo kuhakikisha tunamuongezea mkataba mwingine, hiyo ni baada ya rekodi nzuri aliyokuwa nayo tangu tumkabidhi timu.
“Tangu amekabidhiwa timu, miaka yote timu imeshiriki michuano ya kimataifa ukiachana na kuifunga Simba, hivyo hivi sasa tupo kwenye mazungumzo naye ili kujua vitu gani atakavyohitaji ili viongezwe kwenye mkataba wake mpya,” alisema bosi huyo.
Katika kuthibitisha taarifa hiyo, Championi Jumatano lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Jerry Muro kuzungumzia hilo hakukubali wala kukataa taarifa hizo.
“Pluijm bado ni kocha wetu halali mwenye mkataba na sisi, pia nisingependa kuzungumzia hilo kwa hivi sasa, hilo suala bado halijafika mikononi mwangu,” alisema Muro.
Credit:Salaehjembe
0 comments:
Post a Comment