KIZA kinene! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema ukizungumzia sakata la mkataba mpya wa beki wa kulia wa Simba, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, ambaye hadi sasa amekuwa kwenye figisu figisu na viongozi wa timu yake kuhusiana na suala hilo.
Kessy, ambaye mkataba wake wa sasa na Wanamsimbazi hao umebakia miezi miwili, amekuwa akituhumiwa kuwa msumbufu uwanjani, huku akihusishwa na kipigo ambacho Simba ilikipata kutoka kwa Yanga mwisho wa wiki iliyopita.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba kukubali kufungwa na Watani wao wa jadi mabao 2-0, bao la kwanza lilipatikana baada ya Kessy kufanya uzembe wa kumrudishia mpira kipa Vicent Agban na Donald Ngoma kuuwahi kisha kufunga kirahisi.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata zinadai kuwa baada ya mchezo huo, kumekuwa na shutuma mbalimbali zinazomhusisha Kessy juu ya mchezo huo, huku ikidaiwa kuwa kuna mpango wa beki huyo kutua kwa Wanajangwani msimu ujao.
Taarifa hizo zinadai kuwa kwa kipindi kirefu Yanga wameonyesha nia ya kumhitaji Kessy, lakini beki huyo aliwataka kusubiri hadi mkataba wake umalizike na ndiyo maana viongozi wake wa Simba walipotaka kumuongeza mkataba mpya aliamua kuwatajia dau refu.
“Yanga wanamhitaji Kessy kwa muda mrefu na katika hilo hata alipotakiwa kuongezwa mkataba mpya mara baada ya kurejea kuitumikia timu ya taifa alitaka aongezewe fedha nyingi, hali iliyosababisha hadi sasa kukwama kwa suala hilo.
“Lakini baada ya kutokea uzembe kwenye mechi dhidi ya Yanga, viongozi wameshaanza kumtilia shaka, kwani wameshapewa taarifa za yeye kuanza mazungumzo na Yanga,” alisema mtoa habari.
BINGWA, lilimtafuta Meneja wa mchezaji huyo, Athuman Tippo, ambaye alisema kuwa hadi hivi sasa Simba wamekuwa wagumu kuweka msimamo wao juu ya Kessy, lakini kwa kuwa bado miezi miwili kukamilisha kandarasi yake itajulikana.
“Kila siku Simba wanadai watazungumza naye kesho, keshokutwa, hivi sasa tumeamua kukaa kimya kuwaacha waamue wao na kwa kuwa yule ni mchezaji mahali popote anacheza.
“Tayari zipo timu zimeonyesha nia ya kumhitaji, lakini tunashindwa kutoa jibu la moja kwa moja kutokana na kusubiri kauli ya mwisho ya Simba, lakini ikishindikana anaweza kurejea hata kwenye kikosi chake cha zamani (Mtibwa Sugar),” alisema.
Alisema hivi sasa suala la Kessy kudaiwa kutoonekana mazoezini kwa makusudi halina ukweli, kwani taarifa alizonazo ni mgonjwa na uongozi wake unafahamu hilo.
0 comments:
Post a Comment