KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa Panone mabao 2-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi jioni ya leo.
Shukrani za pekee ziende kwa nyota wawili wa timu hiyo, beki Pascal Wawa na mshambuliaji Allan Wanga waliofunga mabao ya ushindi ya Azam FC baada ya Panone kutangulia kupata bao dakika ya 48 kupitia kwa Godfrey Mbuda aliyepiga kichwa akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Ayoub Masoud.
Mabao ya timu zote mbili yalipatikana kipindi cha pili hasa baada ya mchezo huo kuonekana mgumu sana kipindi cha kwanza kutokana na soka la mipira mirefu sana lililokuwa likitumika kutokana na ubovu wa uwanja.
Mabadiliko ya Azam FC kipindi cha pili ya kuingia viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Jean Mugiraneza na mshambuliaji Kipre Tchetche na kutoka Ame Ally, Frank Domayo na Didier Kavumbagu, yaliwasaidia mabingwa hao kuweza kuwabana Panone kipindi cha pili.
Wawa alifunga bao la kuisawishia Azam FC dakika ya 64 kwa kichwa akimalizia kona safi iliyochongwa na beki Erasto Nyoni, bao ambalo limemfanya afunge bao lake la kwanza ndani ya timu hiyo tokea asajiliwe Desemba mwaka juzi akitokea El Merreikh ya Sudan.
Straika raia wa Kenya, Allan Wanga aliyesota takribani miezi minne bila kufunga bao lolote ndani ya Azam FC tokea alipofunga dhidi ya Stand United Septemba mwaka jana (2-0), yeye alitupia bao la ushindi akimalizia mpira uliotemwa vibaya na kipa wa Panone kufuatia kichwa safi cha Tchetche, aliyeunganisha kona iliyochongwa na Nyoni.
Licha ya Azam FC kupata ushindi huo, imekutana na mazingira magumu sana ya Uwanja wa Ushirika ukiwa mgumu pamoja na vumbi kali lililokuwa likitibuka uwanjani muda wote wa mchezo huo, jambo lililohatarisha afya na usalama wa wachezaji uwanjani.
Kabla ya uwanja huo kutumika kulikuwa na vyupa, vyuma, nondo na takataka nyingi kiasi ambacho kimewafanya wachezaji kucheza kwa takahadhari kubwa ili kuhofia kudondoka na kuumizwa na mabaki ya vyupa vidogo vidogo.
Azam FC hadi inafika hatua ya robo fainali, imefanikiwa kuzitoa timu za African Lyon (4-0), Panone (2-1), mechi zote mbili ikicheza viwanja ya ugenini kuliko timu yoyote iliyofika hatua hiyo.
Kikosi cha mabingwa hao kilichofikia jijini Arusha katika Hoteli ya City Link, kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho asubuhi kwa usafiri wa ndege ya Fast Jet, tayari kabisa kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Yanga utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi hii (Machi 5).
Kikosi cha Azam FC leo:
Aishi Manula, Erasto Nyoni (C), Farid Mussa, Said Morad, Pascal Wawa, David Mwantika, Michael Bolou, Frank Domayo/Jean Mugiraneza dk 61, Ame Ally/Salum Abubakar dk 46, Didier Kavumbagu/Kipre Tchetche dk 45, Allan Wanga
0 comments:
Post a Comment