WAKATI kukiwa na tetesi za Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi kutua Yanga, imeelezwa kuwa mtaalamu huyo ametoa masharti mazito kwa uongozi wa timu hiyo ya Jangwani.
Mwambusi anaonekana kupewa nafasi kubwa kumrithi aliyekuwa kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, ambaye amepewa mkataba wa miezi 18 kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Tangu Mkwasa alipoteuliwa kuinoa Stars kuchukua mikoba ya Mholanzi Mart Nooij, makocha kadhaa wamekuwa wakitajwa kumsaidia Hans van der Pluijm, baadhi yao wakiwa Mwambusi wa Mbeya City, Fred Felix Minziro na wengineo.
Mmoja wa watu wa karibu wa kocha huyo, alisema kuwa, Mwambusi amewapa viongozi wa Yanga masharti ya kuyafanyia kazi kabla ya kufikia makubaliano naye.
Alitaja moja ya sharti hilo kuwa ni Yanga kuonana na uongozi wa Mbeya City kuzungumza nao kwa kina juu ya kuvunja mkataba wa kocha huyo na mambo mengine ya msingi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mbali na sharti hilo, mtoa habari huyo alisema kuwa katika sharti jingine ni kuhakikisha Mwambusi anaiacha Mbeya City katika mazingira salama na kocha atakayechukua nafasi yake awe wa kiwango cha juu.
Credit:Bingwa.
0 comments:
Post a Comment