Na Bertha Lumala, Dar es Salam
MDHAMINI Mkuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, jana imezing'arisha timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu kwa kuzipatia vifaa vipya vyenye thamani ya Sh. milioni 490 kwa ajili ya msimu huu.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa katika hafla iliyofanyika jijini hapa jana huku Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Kelvin Twisa, akisema kutolewa kwa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kimkataba wao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kuhakikisha ligi hiyo inaendeshwa vizuri.
"Kwa niaba ya Vodacom Tanzania, ninazitakia kila la kheri timu zote 16 zinazoshiriki VPL msimu huu. Timu bora na ishinde," amesema Twissa.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa wawakilishi wa klabu zote 16 ni pamoja na jezi za mechi, jezi za mazoezi, mipira, viatu, soksi, vilinda ugoko, nguo za kawaida kwa ajili ya wachezaji na maofisa wa klabu, glavu na vitendea kazi vya waamuzi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB), Boniface Wambura, aliushukuru uongozi wa Vodacom Tanzania kwa kuongeza mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh. bilioni 6.7 kuendelea kuidhamini ligi hiyo.
Wambura aliahidi kuwa bodi hiyo itashirikiana na TFF kuhakikisha ligi inachezwa bila upendeleo kwa baadhi ya timu.
"Timu zimeongezeka kutoka 14 hadi 16, hivyo tutakuwa na mechi 240 msimu huu. Tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na ligi bora kuliko msimu uliopita," amesema Wambura na kueleza zaidi:
"Tumefanyia ufanisi wa waamuzi, si kila refa mwenye 'Class One' (Daraja la Kwanza) anaweza kuchezesha Ligi Kuu. Tutakuwa na waamuzi wachache msimu huu. Tunataka waamuzi bora wenye uwezo wa kutafsiri sheria za soka ili kuwe na 'fair play' (mchezo wa kiungwana)."
Msimu huu wa VPL utaanza rasmi Septemba 12 mwaka huu mabingwa watetezi Yanga wakianzia nyumbani kwa kuwakaribisha Coastal Union.
PICHA: BERTHA LUMALA
0 comments:
Post a Comment