KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, huenda akakipangua kikosi chake kwenye mchezo wao na Simba utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam baada ya kurejea kundini kwa beki kisiki Juma Abdul aliyemaliza adhabu ya kukosa mechi tatu kutokana na kupata kadi nyekundu.
Abdul alionyeshwa kadi hiyo katika mechi ya mwisho ya Yanga msimu uliopita dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.
Kutokana na kurejea kwa Abdul huenda Mbuyu Twite akarudi nafasi ya kiungo mkabaji aliyokuwa akipangwa Thaban Kamusoko ambaye bila shaka atapandishwa kama kiungo mchezeshaji, huku Haruna Niyonzima na Simon Msuva wakitokea pembeni kwenye mchezo wa kesho.
Katika mechi tatu zilizopita, Pluijm alikuwa akimpanga Twite katika nafasi ya beki wa kulia, huku Kamusoko akiwa katikati na Niyonzima akitumiwa kama kiungo mchezeshaji.
Katika mazoezi yao yanayoendelea kisiwani Pemba, Pluijm amekuwa akimpanga Abdul nafasi ya beki wa kulia na kumrudisha Twite katikati na kumsogeza Kamusoko mbele.
“Nipo vizuri sana, nasubiri Septemba 26 uone, najua mashabiki ‘wamemiss’ makrosi yangu kama ya beki wa Barcelona, Dan Alaves… wasiwe na hofu, narudi kwa kishindo watulie waone kazi inavyofanyika siku hiyo,” alitamba Abdul.
Chanzo:Bingwa
Chanzo:Bingwa
0 comments:
Post a Comment