Na Oswald
Ngonyani
Mchezo wa mpira wa miguu maarufu kwa jina la soka bado
umeendelea kuwa mchezo pendwa zaidi kuliko michezo yote inayochezwa juu ya uso
wa dunia. Umaridadi wa wenye kuucheza mchezo huu ni miongoni mwa vitu
vinavyopambiza kuwavutia wengi.
Kunako mchezo huu tayari historia kadha wa kadha
zimekwishawekwa na kuandikwa. Mpaka leo hii kuna wachezaji ambao kwayo walikuwa
gumzo na wameendelea kuwa gumzo tena na tena katika mawanda ya sasa ya
usakataji wa ‘Gozi la ng’ombe’.
Wachezaji wafuatao wameendelea kuwa wa pekee zaidi katika
historia ya mchezo wa soka duniani kote. Hii ni kutokana na makubwa waliyokuwa
wamewahi kuyafanya ndani ya dimba lakini pia wanayoendelea kuyafanya mpaka sasa.
1 Edson Pele (1956-1977) – Brazil
Jina lake kamili ni Edson Arantes do Nascimento. Anashika
nafasi ya kwanza katika orodha ya wachezaji bora wa mpira wa miguu duniani
kuwahi kutokea. Alishinda Kombe la dunia mwaka 1958, 1962 na 1970 ni mchezaji pekee
aliyewahi kushinda kombe la dunia mara tatu.
Akiwa uwanjani alikuwa mchezaji mwenye akili na kasi ya
ajabu. Alikuwa ana uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira na kufunga mabao. Takwimu
zinaeleza kuwa alifunga mabao 1,000 katika kipindi chake cha kucheza mpira.
Heshima yake kwa sasa haielezeki. Amekuwa akialikwa
katika matamasha makubwa ya michezo, hii ni kutokana na namna alivyokuwa
ameifanyia makubwa tasnia ya mchezo wa soka na hata kuwazidi wachezaji wengine
wote, katika nyakati zote.
2. Diego Armando Maradona (1976-1997)-Argentina
Ni mojawapo ya wachezaji waliokuwa na uwezo mkubwa wa
kucheza na kuudhibiti mpira uwanjani. Alifunga goli la ushindi katika fainali
ya kombe la dunia mwaka 1986 dhidi ya Uiengereza goli lililozua utata na kuitwa
“Goli la mkono wa Mungu”
Hakuwa na nidhamu sana uwanjani na hata nje ya uwanja
lakini uwezo wake mkubwa wa kutandaza kandanda dimbani unafahamika na wengi na
atabaki katika kumbukumbu ya wengi sasa na hata siku zijazo.
3. Lionel Messi -Argentina
Ijapokuwa ni mchezaji wa kizazi cha sasa, Muargentina
huyu tayari amekwishafanya makubwa katika historia ya mchezo wa soka tangu
ulipogunduliwa. Ndiye mchezaji bora mara nyingi zaidi wa dunia akiitwaa tuzo hiyo mara nne na hata kuwazidi
wachezaji wengine wote duniani.
Kwa kipindi kirefu sasa ameisaidia sana timu yake ya
Barcelona kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya Hispania huku akizidi
kuendelea kuiletea tija klabu hiyo tena na tena. Alivunja rekodi ya Gerd Muller
ya kufunga mabao 91 katika msimu mmoja mwaka 2012.
Messi ndiye mchezaji pekee aliyewahi kuwa mfungaji bora
katika Ligi ya Washindi Ulaya mara 4 mfululizo. Mbali na sifa zote hizo, Messi
ndiye Mchezaji kijana kufunga mabao 200 katika ligi ya Hispania-La liga.
Mpaka sasa, Lionel Messi anashikilia rekodi ya kuwa Mfungaji
bora wa wakati wote wa klabu yake ya Bcrcelona katika mechi rasmi za klabu yake
hiyo. Nidhamu yake ya hali ya juu katika soka inamfanya aendelee kuwa juu ya
wengine na hata kujikuta akizidi kukumbukwa zaidi.
4. Johan Cruyff (1964-1984)-Uholanzi
Mdachi aliyeichezea Ajax na Barcelona katika miaka ya 60
na 70. Alijulikana kama mchezaji bora wa ulaya wakati huo. Alikuwa mahiri zaidi
katika mfumo wa “Total Football”
ambapo wachezaji wanabadirishana nafasi wakati wa kupeana pasi na kuwafanya
wachezaji wote wa timu kushiriki.
Alipata tuzo 3 za mchezaji bora wa ulaya na kushinda
vikombe 8 akiwa na klabu yake hiyo ya Ajax.
5. Franz Beckenbauer (1964-1984)-Ujerumani
Aliichezea kwa mafanikio makubwa klabu ya Bayern Munich
ambapo akiwa klabuni hapo alifanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu ya nchini humo
(Bundesliga) mara tano na kombe la ulaya mara tatu. Alikuwa na uwezo wa kucheza
nafasi nyingi uwanjani hasa nafasi ya ulinzi na ushambuliaji.
6. Alfredo Di Stéfano (1943-1966) – Argentina/Hispania
Alifunga mabao katika mashindano ya ulaya mara tano
mfululizo. Alichezea klabu ya Real Madrid katika miaka ya 50 na kuwika sana.
7. Ferenc Puskás (1944-1966) -Hungaria
Mojawapo ya wafungaji bora wa magoli kuwahi kutokea
duniani ijapokuwa hajulikani sana kwa wengi. Alikuwa na wastani wa angalau goli
moja katika kila mechi aliyocheza.
Alikuwa mchezaji wa timu ya taifa Hungaria na klabu ya
Real Madrid ya nchini Hispania. Alifunga magoli 7 katika fainali mbili za ubingwa
barani ulaya.
8. Cristiano Ronaldo -Ureno
Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao. Mwaka
2014 alitimiza mabao 400 akiwa na umri wa miaka 28 tu. Ana uwezo wa kumiliki
mpira stamina na anajua goli lilipo. Ndiye mchezaji bora wa dunia kwa sasa
akiwa ameitwaa tuzo hiyo katika awamu tatu tofauti, na anapewa nafasi ya kufanya
hivyo zaidi kwa miaka ijayo.
Kwa sasa ndiye mpinzani nambari moja wa Lionel Messi.
Inasemekana kuwa ukulu wao katika soka huenda ukawafanya wazidi kubadilishana
katika kinyang’anyiro hicho cha tuzo za Ballon D’ Or kila mwaka. Kwa sasa
anakipiga katika klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania.
9. Zinedine Zidane ‘Zizzou’ -Ufaransa
Kwa wengi anajulikana kwa jina la ‘Babu’. Alistaafu
kucheza kandanda mwaka 2006 mara baada ya tamati ya fainali za Kombe la dunia
huku familia ya mchezo wa soka ikionekana kutoridhika kwani alistaafu akiwa
bado na kiwango cha hali ya juu.
Alifunga magoli lukuki akiwa na Real Madrid na kuisaidia
timu yake kufanya vizuri katika ligi na hata katika ubingwa wa ulaya. Kwa sasa
ni miongoni mwa wahusika wa benchi la ufundi la klabu hiyo tajiri duniani.
10.Eusébio (1958-1978)-Ureno
Kwa kizungu aliitwa “The Black Panther” yaani “Paka Pori
Mweusi” toka Ureno. Alizaliwa Msumbiji na kucheza soka nchini Ureno. Inasemekana
kuwa kabla ya Cristiano Ronaldo (CR7) alitambulika kuwa mchezaji bora zaidi kuwahi
kutokea nchini Ureno.
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment