Ungozi wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting umesema unasikitishwa na klabu ya Toto Africans ya jijini Mwanza kwa kumsajili mchezaji Hamis Seleman wa Ruvu Shooting ambaye bado anamkataba halali na Ruvu Shooting ambayo itacheza ligi daraja la kwanza inayotarajia kuanza hivi karibuni kutokana na kushuka daraja kutoka ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita.
Afisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire ameelekeza lawama zake moja kwa moja kwa klabu ya Toto Africans ambayo inajiandaa kwa ligi kuu Tanzania bara msimu ujao kufuatia kufuzu kucheza ligi hiyo ikitokea ligi daraja la kwanza.
Bwire amesema, Toto imemsajili mchezaji wao halali ambaye anamkataba na Ruvu Shooting na amekuwa akilipwa mishahara na klabu hiyo hata baada ya kusaini mkataba na Toto kinyemela bila Ruvu Shooting kujua, alitumiwa mshahara kutoka Ruvu Shooting na kuutumia.
“Klabu ya Ruvu Shooting inasikitishwa na kitendo cha timu ya Toto Africans ya Mwanza kumrubuni na kumsainisha mkataba kinyume cha sheria mchezaji wake Hamis Seleman”, Bwire amesema.
“Hamis Seleman ni mchezaji halali wa Ruvu Shooting na ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na kuwasilishwa TFF.
“Ruvu Shooting imemlipa mshahara kipindi chote hata mwezi uliopita akiwa likizo, alitumiwa mshahara wake akaupokea kumbe tayari alikuwa amesainishwa mkataba kinyemela na Toto bila uongozi wa Ruvu Shooting kujua”.
“Ruvu Shooting tunaiomba klabu ya Toto imuachie mchezaji wetu au kama inamuhitaji uongozi uje tuzungumze na tukubaliane, vinginevyo barua ya pingamizi tuliyokwishaiandaa tutaiwasilisha sehemu husika muda wa kufanya hivyo ukifika”.
“Hii itamuweka pabaya kijana kwa kuwa na mikataba na timu mbili tofauti”.
0 comments:
Post a Comment