Uongozi wa Simba unaamini kwa dhati na kwa vitendo dhima ya ukweli na uwazi katika utendaji wake. Katika kipindi cha wiki chache zilizopita klabu yenu ya Simba ilianza mchakato wa kumsajili mchezaji Laudit Mavugo kutoka Vital’O ya Burundi. Uongozi wa Simba katika kuhakikisha jambo hili linafanikiwa ilianza mawasiliano rasmi na klabu ya Vital’O ambapo walitoa matakwa yatuatayo;
1. Tulikubaliana baada ya majadiliano ya awali kuwa mchezaji asajiliwe kwa Tsh 110 milioni.
2. Kumwacha mchezaji amalize ligi na kombe la FA.
Baada ya mawasiliano na makubaliano ya awali, klabu ya Simba ilimtuma Makamu wa Rais Geofrey Nyange ili kukamilisha majadiliano na uongozi wa Vital’O ili kukamilisha usajili wa Laudit Mavugo. Baada ya mjadala mrefu Vital’O walitaka yafuatayo;
1. Kuongeza mara dufu thamani ya mchezaji huyo na pia kuongeza vipengele vipya vya mauzo kinyume na makubaliano ya awali.
Thamani mpya ya mchezaji imepandishwa na kuwa Tshs 200 milioni kutoka ile ya awali ya Tsh 110 milioni ambazo zilijumuisha gharama za kumlipa mchezaji.
2. Aidha kumeibuka mzozo mpya Kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, klabu inayodai kumlea Mavugo na kudai hati miliki ya mchezaji huyo.
3. Licha ya mkanganyiko wa umiliki wake, Vital’O imedai kuwepo kipengele kipya kinachodai mapato ya asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Simba SC kwenda klabu nyingine.
Pamoja na juhudi ya dhati za kumsajili Laudit Mavugo ikiwa ni pamoja na kutuma Viongozi na mijadala mirefu, kutokana na changamoto hizo, gharama kubwa na uzoefu tuliopata kutokana na usajili tata wa kimataifa tulizopitia, Simba SC imeamua kusitisha rasmi usajili wa Mavugo . Wakati mchakato huu ukiendelea Simba SC ilikuwa inaendelea na mazungumzo na washambuliaji kadhaa wa kimataifa Ili kuwa na wigo mpana wa kuchagua.
Tunaamini tutasajili mchezaji mzuri na bora ambaye thamani na uwezo wake utashabihiana au kuwa zaidi.
Pamoja na changamoto ya usajili wa Mavugo, tunayofuraha kuwajulisha kuwa Simba SC imekamikisha usajili wa beki wa kimataifa wa Burundi kutoka klabu ya Vital’O Emery Nimubona ambaye anawasili nchini Jumapili tarehe 2 August 2015 na atajiunga na kambi huko Zanzibar.
Uongozi wa Simba utaendelea kuwapa taarifa rasmi na uhakika kuhusu timu yenu.
Taarifa hii imetolewa na mtandao wa Simba SC simbasports.co.tz
0 comments:
Post a Comment