Ivo (kulia) alikuwa mwalimu mzuri wa Manyika Peter Jr (kushoto)
Wekundu wa Msimbazi Simba SC, rasmi wameachana na golikipa
wao mkongwe, Ivo Philip Mapunda wakidai kwamba hakutoa ushirikiano wakati
alipotakiwa kusaini mkataba mpya.
Taarifa zilieleza kwamba Ivo alikabidhiwa Shilingi Milioni
10 kwa ajili ya kuanguka mkataba mpya, lakini hajatokea licha ya kutafutwa na
viongozi wa Simba.
Ivo amekiri kutopewa mkataba na uongozi wa Simba baada ya
kuonana nao kwa mazungumzo zaidi.
“Nimeambiwa sikuonyesha ushirikiano wakati natakiwa kwenda
kusaini fomu, wamesitisha mkataba kwasababu hiyo, wanadai kiongozi aliyepewa jukumu
hilo alinitafuta sana na akapeleka taarifa kwamba sitoi ushirikiano, kwahiyo
hawajanipa”. Amesema Ivo.
Hata hivyo imeelezwa kwamba viongozi wa Simba wamemtaka
mlinda mlango huyo kurejesha fedha alizochukua ambazo zinadaiwa kuwa milioni
10.
“Nimeambia nirejeshe fedha nilizochukua, mimi nimesema sawa,
sihitaji mgogoro, nataka nitoke Simba salama, kama wao wanahitaji nirudishe
pesa yao, nitarudisha”. Amefafanua Ivo na kuongeza: “Nilipochukua pesa
nilifanyia biashara, pale nitakapoipata nitarudisha, lakini siwezi kusema nitarudisha
lini”.
Je, ni kweli alichukua milioni 10?Ivo amesema: “Siwezi
kusema ni shilingi ngapi, siwezi kuweka mambo hadharani, hayo ni maneno tu,
mimi ninachosema ni kwamba nitarudisha
nitakapoipata”.
“Kitu kizuri inatakiwa usiwe mropokaji, nitakapoipata
nitarudisha, labda kitu ninachoweza kuwa muwazi ni kwamba sina kinyongo”
“Nawashukuru sana wanasimba, walinipa sapoti nilipokuwa nafanya
vizuri na vibaya, nawatakia kila la kheri, katika maisha ya mpira, mlango mmoja ukifungwa mwingine unakuwa wazi”
Nao Simba wamekiri kuachana na Ivo baada ya kushauriana na
kocha wa makipa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara
amesema: “Kimsingi tulikuwa na kikao kizuri na cha kuungwana na Ivo, baada ya kushauriana
na mwalimu wa magolikipa, kocha ameridhika kabisa na uwezo wa magolikipa waliopo
kwa maana ya Vicent Angban kutoka Ivory Coast na magoli wetu chipukizi Peter
Manyika na Dennis Richard. Ivo tumeachana naye kwa amani”.
“Kuhusu kuambiwa kurejesha fedha, mimi sijaambiwa taarifa
hiyo na viongozi. Kama Ivo kasema hivyo, hiyo inaweza kuwa taarifa rasmi, ila
mimi sijaambiwa”. Amesema Manara.
0 comments:
Post a Comment