Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Kiungo aliye kwa mkopo katika klabu ya Simba SC, Joseph Kimwaga amekiri wazi kuwa alikata tama ya kucheza mpira baada ya mambo kuwa magumu katika klabu ya Azam FC. Kimwaga licha ya kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Azam FC alisumbuliwa na majeraha ya goti kiasi cha kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini.
Mchezaji huyo anayetumia mguu wa kushoto, anakumbukwa na wapenzi wengi wa mpira nchini kutokana na kufunga goli la ushindi katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Novemba, 2013 wakati Azam iliposhinda 3-2.
“ Baada ya kuumia na kuwa nje kwa muda mrefu nilianza kukata tama kama kweli ningeweza kurudi katika kiwango change cha kawaida. Kusajiliwa na Simba nitachukulia kama njia ya kurejesha makali yangu” anasema Kimwaga wakati nilipozungumza naye kwa njia ya simu akiwa kambini Zanzibar na timu hiyo.
Samba imekuwa Zanzibar kwa kambi ya mwisho kabla ya kuanza kwa ligi kuu Septemba 12, itacheza na JKU ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki siku ya Jumapili hii. Kimwaga tayari amecheza mchezo mmoja wa maandalizi wakati timu hiyo ilipotoka suluhu-tasa na URA ya Uganda wiki iliyopita anatajwa kama mtu wa kuchukua nafasi ya iliyoachwa na winga Ramadhani Singano ambaye amejiunga na Azam FC.
“ Nipo hapa kufanya kazi, lengo langu ni kushirikiana na wenzangu kuisaidia Simba msimu huu. Najifua ili kumshawishi mwalimu nipate nafasi ya kucheza mara kwa mara. Unajua nimekuwa nje ya uwanja kwa mwaka mzima kutokana na majeraha. “ anasema Kimwaga ambaye tangu amepona hakuwahi kuichezea Azam FC katika gemu ya ushindani.
0 comments:
Post a Comment