Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
USHINDI wa magoli 2-0 dhidi ya KMKM ambao Yanga imeupata leo huku Gor Mahia FC ikishikwa kwa sare 1-1 dhidi ya Al Khartoum FC unazifanya timu hizo tatu ziwe hatarini kuangukia mdomoni mwa APR FC ambayo imepania kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka huu.
APR FC iliungana na timu hizo tatu pamoja na Azam FC na Al Shandy ya Sudan, kutinga robo fainali baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya LLB FC ya Burundi katika mechi yao ya mwisho ya Kundi B iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
APR iliyoshinda 1-0 dhidi ya Al Shandy na 2-0 dhidi ya Heegan katika mechi mbili za mwanzo za Kundi B, sasa inasubiri moja kati ya Yanga, Gor Mahia na Al Khartoum kukabiliaana nayo katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Dakika ya 53 mshambuliaji mtokeabenchini Nahimana Abdoul Aziz alifunga bao la LLB akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia ndani ya boksi mpira wa krosi iliyotemwa na kipa Ndoli Claude kutoka wingi ya kushoto iliyomiminwa na Kiza Fataki.
Bao hilo lilidumu kwa dakika tano tu kwani dakika mbili kabla ya saa ya mchezo, winga hatari wa APR Sibomana Patrick aliisawazishia timu yake kwa mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Martin Saanya wa Tanzania kutokana na beki wa kati na nahodha wa LLB, Hakizimana Issa kuunawa mpira ndani ya boksi.
YANGA 2-0 KMKM
Mabao ya Yanga katika mechi yao ya leo ya Kundi A dhidi ya KMKM yalifungwa na washambuliaji Malimi Busungu dakika ya 57 likiwa ni goli lake la tatu na Amissi Tambwe dakika 75.
Timu itakayomaliza nafasi ya kwanza katika kundi hilo la A, itamenyana na 'Best Loser', mshindi wa pili ataivaa timu itakayomaliza nafasi ya kwanza katika Kundi C linaloongozwa na Azam FC kwa sasa ikiwa na pointi sita baada ys kushinda mechi zote mbili za awali.
Timu itakayomaliza nafasi ya tatu Kundi A, itamkabili timu iliyomaliza kileleni mwa Kundi B, APR FC ambayo ilitinga fainali mbili zilizopita za Kombe la Kagame na kufungwa dhidi ya Vital'O na El Merreikh michuano hiyo ilipofanyika Sudan na Rwanda.
Yanga sasa inakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi sita, moja nyuma ya vinara Khartoum na Gor Mahia ambao wote wana pointi saba.
Yanga huenda pia ikakumbana na muziki mnene wa kuikabili Azam FC ikiwa timu hiyo ya Jangwani itamaliza nafasi ya pili na Azam Wanalambalamba wakamaliza katika nafasi ya pili pia Kundi C.
0 comments:
Post a Comment