Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Meneja uhusiano wa umma wa MultiChoice Tanzania, BARBARA Kambogi, amesema timu itakayotwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu itazawadiwa Sh. milioni 59.1.
Aidha, kampuni hiyo ambayo itakuwa inarusha moja kwa moja matangazo ya mechi zote za mashindano hayo yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia kesho kupitia kituo chake cha SuperSport, itakuwa inatoa zawadi kwa mchezaji atakayeng'ara zaidi katika kila mechi.
Barbara amesema: "Bingwa atazawadiwa pesa taslim shilinhi milioni tatu za Kenya (sawa na Sh. milioni 59.1 za Tanzania), mshindi wa pili atapata shilingi milioni mbili za Kenya (Sh. milioni 39.4 za Tanzania) wakati mshindi wa tatu atazawadiwa shilingi milioni moja za Kenya (Sh. milioni 19.7 za Tanzania)."
"Pia kutakuwa na zawadi nzuri kwa nyota watakaong'ara katika michuano hii ya CECAFA zikiwamo za Mchezaji Bora wa Msahindano, Mfungaji Bora, Kipa Bora, Beki Bora na Kiungo Bora ambao pia alisema watapewa ving'amuzi vya DStv Explora," amesema zaidi Barbara na kueleza kuwa Mchezaji Bora wa kila mechi watampa zawadi ya king'amuzi cha kisasa cha DStv cha 'Zappa Box' chenye picha zenye kiwango cha juu, yaani HD.
Amesema matangazo yatakuwa katika lugha mbili, watangazaji Bernard Otieno, Jacob Mulee na Mark Ssali 'wataruka hewani' katika lugha ya Kiingereza wakati Ali Salim Mmanga, Cliff Ndimbo na Michael Were watatangaza kwa lugha ya Kiswahili.
Mabingwa mara tano na wenyeji, Yanga wamepangwa Kundi A pamoja na mabingwa wa Kenya, Gor Mahia, Khartoum ya Sudan, Telecom ya Djibouti na KMKM ya Zanzibar.
Wanafainali wa mwaka jana, APR ya Rwanda wako Kundi B pamoja na Al Ahly Shandy, LLB ya Burundi na Elman ya Somalia.
Mabingwa wa Uganda, KCC wako Kundi C pamoja nna Malakia ya Sudan Kusini, Azam (Tanzania) na Adama City ya Ethiopia.
0 comments:
Post a Comment