Admini wa Ukurasa maarufu wa facebook wa 'Naipenda Yanga' ameandika maneno mazito na yenye mantiki akiwashauri viongozi wa Yanga kuwa na mikakati madhubuti na klabu yao, ikiwemo kutumia vizuri vipaji kutoka timu yao ya vijana, lakini vile vile matumizi mazuri ya pesa katika usajili hasa kwa wachezaji kutoka nje ya nchi. Ushauri huu si tu kwa Yanga bali ni kwa vilabu vyote vya Tanzania.
Soma mwenyewe hapa jinsi alivyotiririka;
"Naangalia kikosi changu cha Yanga nafurahi kuona kimesheheni wachezaji nyota karibu katika kila nafasi uwanjani,nafurahi zaidi nnapopata taswira ya viwango vyao kweli ni wenye vipaji haswa,kuna kitu nagundua katika kikosi chetu cha wakubwa naamua kurejea vikosi vya miaka iliyopita kuanzia mwaka 2000 hadi sasa dakika chache baadaye napata masikitiko kuhusu mustakabali wa wadogo zangu wa Yanga chini ya miaka 20 na wadogo zao.
Miaka inakatika tu na tambo zetu huku tukiwa tumefeli kwa kiwango kikubwa kuiendesha klabu yetu katika taswira ya kimataifa kama tunavyojiita wa kimataifa,angalau ingekuwa hatuna uwanja wa mechi lakin hatuna hata uwanja wa mazoezi leo tupo huku kesho kule.Kubwa lingine sera mbovu za usajili iwe kusajili ama kuuza mchezaji,fumbia macho jinsi tunavyokosa mamilioni ya kuuza wachezaji nje,jiulize zaidi ya miaka 15 sasa mchezaji yupi tuliyemuandaa na kumkuza toka timu zetu za vijana?mbaya zaidi inaonekana kwa miaka mingine mingi ijayo tusitegemee vijana wa kutoka under 20 wakaichezea timu ya wakubwa kwa mafanikio hakuna mipango hiyo thabiti,hakuna.
Hata magolikipa sisi tunanunua katika vilabu vya daraja la kwanza,superstar anayechipukia Geofrey Mwashiuya tumemtoa Mbozi huko ligi daraja la kwanza inasikitisha sana kuona takribani miaka 13 imepita toka Edibily Lunyamila aondoke Jangwani leo watu wanajinasibu kumpata Lunyamila mpya,inasikitisha kwa kuwa hakuna dhana thabiti ya vijana kutoka timu za wadogo kuja kurithi nafasi katika timu kubwa.Mrisho Ngassa kacheza yanga muda mrefu lakini alipoondoka tu tukaanza kuumiza kichwa nani awe mrithi wake,hakuna aliyejaribu kutupia jicho kwenye kikosi cha Salvatory Edward na kuanza kumwandaa mrithi mapema.
Leo hii tunatambua haswaa magwiji wetu Nadir Haroub na Kelvin Yondani wanaelekea kuchoka,je tumejiandaa kuandaa warithi wenye uzalendo wa kweli kama alionao Nadir?hakuna,tunasubiri muda umtupe mkono zaidi ndipo tugundue tumechelewa.Hata Pato Ngonyani tumemtoa Majimaji FC . . Kuna kijana anaitwa Issa Ngao ni mmoja wa mabeki mahili kwa siku za usoni lakini siasa zetu zinazidi kumtenga na Yanga,nasikitika kusikia yule mfungaji bora wa Under 20,Notkely Masasi alishatimkia Kenya na anafanya vizuri huko bila klabu yetu kunufaika.
Tunafurahia usajili wa wachezaji kutoka vilabu vingine ndio maana sishangai tunabeba hata magalasa tena kwa bei kubwa sana sababu hatuangalii mahitaji yetu halisi na falsafa ya klabu yetu kwa ujumla.Tungekuwa tunawatumia vema magwiji wetu Ally Mayai,Edibily Lunyamila,Salvatory Edward,Mohamed Hussein Mmachinga tusingepoteza muda wa kuhangaika na akina Maurice Sunguti,Kenneth Asamoah,Steven Bengo wala tusingedanganywa na Maximo kuhusu wajomba zake JAJA na Emerson.Mmeshuhudia wenyewe Shadrack Nsajigwa katuletea Mwashiuya kwa milioni 7 tu na mshahara wa Mwashiuya usiozidi milioni 1 huku klabu yetu ikitumia zaidi milioni 80 na mshahara zaidi ya milioni 5 kumlipa Coutinho anayesugulishwa benchi na Mwashiuya.Thamani ya kikosi kizima cha Gor Mahia ni sawa na thamani ya Haruna Niyonzima na Donald Ngoma pekee.
Tunatumia gharama kubwa kuhudumia wachezaji wetu wa timu za vijana lakini finishing yetu ili kupata mchango wao katika yanga ya wakubwa imekuwa mbovu,matokeo yake tunazinufaisha timu za Ndondo tu.Je unaikumbuka ile Yanga iliyopewa jina la Black Stars?iliyobeba ubingwa wa bara,muungano na kufika hatua ya makundi klabu bingwa Afrika?ni matunda ya uwekezaji katika timu yetu ya vijana.
Sipendi Yanga iwe genge la wachezaji wasiofaa kuja kujipigia pesa na kuondoka,hizi hela tunazopoteza kwa kufanya usajili wa fasheni pasipo kuzingatia "proffesionalism" tungeweza kufanyia maendeleo kama tungekuwa na mipango thabiti ya kuifikisha Yanga mbali.
Nakutakia asubuhi njema"
Admin Hissan Salum Iddi.
0 comments:
Post a Comment