Kwa kuzingatia marekebisho ya Kanuni ya Ligi Daraja la Pili (SDL) yaliyofanywa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) hivi karibuni, SDL kwa msimu wa 2015/2016 itachezwa katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Timu itakayoongoza kundi itacheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2016/2017 wakati ya mwisho katika kila kundi itarudi kucheza Ligi ya Mkoa wake kwa msimu wa 2016/2017.
Makundi ya SDL ni kama ifuatavyo; Kundi A ni Abajalo FC (Tabora), Singida United (Singida), Mvuvuma FC (Kigoma), Milambo FC (Tabora), Green Warriors (Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam).
Timu zinazounda kundi B ni Bulyanhulu FC (Shinyanga), JKT Rwamkoma (Mara), Pamba FC (Mwanza), AFC Arusha, Madini FC (Arusha) na Alliance Schools (Mwanza).
Kundi C ni Kariakoo (Lindi), Mshikamano FC (Dar es Salaam), Cosmopolitan (Dar es Salaam), Abajalo FC (Dar es Salaam), Changanyikeni Rangers (Dar es Salaam) na Villa Squad (Dar es Salaam).
Nazo African Wanderers (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Town Small Boys (Ruvuma), Wenda FC (Mbeya), Coca-Cola Kwanza FC (Mbeya) na Sabasaba United (Morogoro) zitakuwa kundi D.
Klabu nyingi bado hazijatuma jina la uwanja wa nyumbani, hivyo zinakumbushwa kufanya hivyo haraka ili kurahisisha upangaji wa ratiba.
Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu wa 2015/2016 inatarajia kuanza Oktoba 17 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment