Wachezaji wa timu ya Khartoum ya Sudan wamekuwa wakinywa maji kwa kutumia vikombe wakati wa mazoezi yao kitu ambacho kilizua maswali mengi kwa baadhi ya wadau wa soka waliokuwa wakifuatilia mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume.
Timu hiyo ambayo inasemekana ni moja ya timu zenye pesa nyingi nchini Sudan ikiwa inanolewa na kochwa mghana Kwesi Appiah ambaye aliiongoza timu ya taifa ya Ghana kwenye michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Brazil mwaka 2014 lakini timu hiyo ilitupwa nje ya michuano hiyo kwenye hatua ya makundi.
Mtandao huu ulilazimika kufanya mahojiano na moja ya mchezaji wa timu ya Khartoum, Salah Eldin Osman Bilal ambaye ni nahodha wa kikosi hicho ili kubaini kwanini wanashirikiana vikombe kunywa maji, hawana uwezo wa kununua maji ya chupa au nini kinasababisha wafanye hivyo.
“Huu ni utamaduni wetu sisi wasudani, sio kama hatuna pesa, hayo maji yenyewe unayoyaona ni maji ya kwenye chupa lakini kilichofanyika ni kuyamimina kutoka kwenye chupa na kuyaweka kwenye chombo kimoja ambacho tutatumia vikombe kunywa”, alifafanua.
“Hii ni ishara ya upendo, umoja na mshikamano na tunafurahia kunywa maji kwa kutumia vikombe. Wakati mwingine hata mwenzio anapobakiza maji kwenye kikombe hutakiwi kuyamwaga, unayanywa halafu kama unakuwa bado haujatosheka unachota mengine unakunywa mpaka kiu inakaika”, aliongeza.
“Hapa watu wanaweza wakatushangaa, lakini kwenye ligi ya kwetu tunafanya hivi hadi kwenye mechi tunapokuwa uwanjani na hii haimaanishi kuwa hatuna pesa ya kutosha kununua maji ila ni utamaduni wetu tu”, alisisitiza.
Kikosi cha Khartoum jana kilikata tiketi ya kucheza robo fainali ya Kagame Cup baada ya kuitungua KMKM ya Zanzibar kwa goli 2-1 na sasa wao ndio wanaoongoza kundi A wakiwa na pointi sita na magoli saba ya kufunga wakifuatiwa na Gor Mahia wenye pointi sita pia lakini wanatofautishwa na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa. Yanga wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu sawa na KMKM lakini nao wanatofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa wakati Telecom wako mkiani mwa kundi hilo wakiwa hawana pointi.
0 comments:
Post a Comment