Wakati hekaheka za usajili wa wachezaji na makocha ukiendelea kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi, timu ya Ndanda FC ‘Mtwara Kuchele’ imeamua kumuonesha mlango wa kutokea kocha wao Jumanne Chale na nafasi hiyo inashikiliwa na Hamidu Mawazo ili kukidhi vigezo vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa timu zinazoshiriki michuano ya ligi kuu Tanzania bara.
Idrisa Bandari ni msemaji wa Ndanda FC ametanabaisha kuwa, timu yao imeamua kumtema kocha huyo kabla hata ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu kuanza kwakuwa sheria ya TFF inataka makocha watakaozifundisha timu zinazoshiriki ligi hiyo kuwa na leseni ya ukocha ya daraja A au B inayotambuliwa na CAF wakati Jumanne Chale analeseni ya daraja C.
Hata hivyo Bandari amesema, Mawazo atakuwa ni koha wa muda tu kutokana na kutingwa na shughuli nyingi na atakifundisha kikosi hicho kwa kipindi ambacho Ndanda watakuwa wakitafuta kocha mpya.
Kuhusu usajili Bandari amesema, wameshafanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji wa zamani wa Kagera Sugar na timu ya Taifa Atupele Green akiwa ni miongoni mwa wachezaji wapya 10 waliosajiliwa na timu hiyo.
Wachezaji wengine waliosajiliwa na Ndanda FC ni pamoja na Dickson Mganda (Kagera Sugar), Aman Juma (Coatal Union), Salvatory Mkebe na Juma Nabe (Ruvu Shooting), Ibrahim Mamba (Tanzania Prisons), Ahamad Msimu (Mtibwa Sugar), Shadrick Frederick (Simba B).
0 comments:
Post a Comment