Tuesday, July 28, 2015

VIGOGO wa Cecafa hawakutamani timu wenyeji zikutane kabla ya hatua ya nusu fainali, lakini kwa sasa haizuiliki, Yanga na Azam lazima zicheze robo fainali kesho Jumatano kwenye michuano ya Kombe la Kagame na mmoja wao lazima aondoke kwenye mashindano.
Lakini si hivyo tu, Azam haikutaka kukutana na Yanga kwenye michuano hiyo kwenye hatua ya mtoano. Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema: “Unapocheza na Yanga unacheza dhidi ya mashabiki zaidi ya 45,000 na pia waamuzi na baadhi ya maofisa, hiyo inaufanya mchezo kuwa mgumu zaidi, tutapambana ili kuweza kupata matokeo mbele ya changamoto hizo, sikupenda kukutana na Yanga katika hatua za mwanzoni, lakini ndiyo imeshakuwa hivyo.”
Katika Kagame ya msimu huu, Azam ndiyo yenye rekodi ya kuvutia ikiwa imeshinda mechi zake zote za makundi na haijafungwa hata bao moja. Pia safu yake ya ushambuliaji inatisha kwa kufunga mabao manane. Ndiyo yenye wastani mzuri kati ya timu 13 zinazoshiriki.

Mechi ya kesho pale Uwanja wa Taifa itakuwa ya nne katika michuano ya Kagame. Ni pambano gumu litakalokuwa na upinzani mkali na Hall anaamini kuwa moto walioanza nao kwenye michuano hiyo ndiyo utakaowachoma na Yanga.

Lakini kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, amesema hatishwi na rekodi tamu za Azam, badala yake amekiandaa kikosi chake kwa mechi ya nusu fainali kwani ana hakika ya ushindi katika mchezo huo.

Pluijm alisema hatishiki na rekodi ya Azam ambayo katika mechi tano za mwisho walizokutana nao Jangwani wamecheka mara moja, badala yake akawahamasisha mashabiki wa Yanga kujiandaa kusherehekea ushindi mapema.

Kocha huyo Mdachi alisema anafahamu kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na timu hizo mbili kufahamiana na kucheza michezo mingi pamoja, lakini ana imani kubwa kikosi chake kitashinda na kutinga hatua ya nusu fainali.

Yanga imelazimika kukutana na Azam katika hatua hiyo baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kumaliza wakiwa washindi wa pili wa Kundi A wakati Azam imemaliza ikiwa mshindi wa kwanza wa Kundi C.

Mechi hiyo inakuwa ni marudio ya fainali ya Kombe la Kagame ya mwaka 2012 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 na nyota wa mchezo huo akiwa Said Bahanuzi aliyetemwa na Yanga hivi karibuni baada ya Pluijm kudai kwamba ana masihara uwanjani.

Pluijm aligoma kuweka wazi mfumo atakaoutumia katika mchezo huo kuikabili Azam ambayo inatumia mfumo wa 3-5-2 ambao umeiwezesha timu hiyo kushinda mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao hata moja.

“Kuhusu mfumo nitakaotumia siwezi kusema, hiyo itakuwa ni siri yetu,” alisema

Kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’ amewataka wachezaji wote wa timu hiyo kuwa makini kwani Azam siyo timu ya kubeza na lolote linaweza kutokea katika mchezo huo.
Barthez ambaye aliibuka mchezaji bora wa mechi ya juzi Jumapili dhidi ya Al Khartoum ya Sudan alisema mchezo huo utakuwa mkali kutokana na timu hizo kufahamiana huku akikiri kuwa Azam imekamilika kila idara na si safu ya ushambuliaji pekee.

Kwa upande wa kocha Hall ameonyesha wasiwasi wa kukutana na Yanga katika hatua ya robo fainali kwa madai kuwa timu hiyo ina mashabiki wengi na pia baadhi ya maofisa wa Cecafa wangependa kuiona ikifika mbali.

Hata hivyo kocha huyo alisisitiza kuwa timu yake itapambana kufa na kupona kuhakikisha wanapata ushindi.

Achana na michezo ya Ngao ya Hisani ambazo timu hizo zimekutana au fainali ya Kombe la Kagame la mwaka 2012 au ile ya Kombe la Mapinduzi, Yanga na Azam katika Ligi Kuu imekutana mara 14 na hakuna mbabe kati yao kuonyesha namna gani pambano la kesho ni presha presha.

Katika mechi hizo 14 za Ligi Kuu tangu mwaka 2008, Yanga na Azam kila moja imeshinda mara tano na kuambulia sare nne, ingawa katika mechi tano zilizopita za Ligi Yanga imenyanyasika mno kwa kupoteza mechi mbili dhidi moja ya Azam na michezo miwili zilienda sare. Kitu cha kustaajabisha ni kwamba katika mechi hiyo 14 timu hizo zinatofautiana wastani wa bao moja tu la kufungwa na kufungwa, Yanga ikiwa na mabao 20 dhidi ya 19 ya Azam.

Rekodi zao Ligi Kuu

Mei 6, 2015

Yanga 1-2 Azam

Desemba 28, 2014

Azam 2-2 Yanga

Machi 19, 2014;

Yanga 1-1 Azam
Septemba 22, 2013;

Azam 3-2 Yanga

Februari 23, 2013;

Yanga 1-0 Azam

Novemba 4, 2012;

Azam 0-2 Yanga

Machi 10, 2012;

Yanga 1-3 Azam

Septemba 18, 2011;

Azam 1-0 Yanga

Machi 30, 2011;

Yanga 2-1 Azam
Oktoba 24, 2010;

Azam 0-0 Yanga

Machi 7, 2010;

Yanga 2-1 Azam

Oktoba 17, 2009;

Azam 1-1 Yanga

Aprili 8, 2009;

Yanga 2-3 Azam

Oktoba 15, 2008;

Azam 1-3 Yanga
Chanzo:Mwanaspoti

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video