Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
BAADA ya jana kumwangalia mshambuliaji Gaudence Mwaikimba, leo katika safu hii ya wasifu wa mchezaji anayecheza Tanzania, tunamwangalia winga wa Yanga, Simon Msuva.
Aliibuka Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita.
DONDOO ZA MSUVA
Kuzaliwa: Oktoba 2, 1993
Mahali: Dar es Salaam
Timu alizowahi kuchezea: Azam FC (2010-2011), Moro United (2011-2013), Yanga 2013 hadi sasa.
Mataji makubwa: Mfungaji Bora wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara (2014-2015 - alifunga magoli 17), Mfungaji Bora Kombe la Mapinduzi 2015 - magoli matano. Mfungaji Bora Uhai Cup 2010.
Aliwahi kuwa dansa wa kundi la THT 2004 - 2005.
Alikotoka
Kutokana na kuwa vipaji viwili na vyote akiamini kuvimudu vilivyo, 2006 Msuva alijiunga na timu ya mchangani inayojihusisha na ukuzaji wa vipaji vya vijana wadogo ijulikanayo kwa jina la 'Wakati Ujao'.
Akicheza kama mshambuliaji wa kati na wakati mwinge winga, Msuva alijiunga na timu ya kukuza vipaji vya vijana ya Azam 2008 ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa.
Avunjika
Ndoto zake za kucheza soka nusura zifikie ukingoni baada ya kuvunjika mguu mwishoni mwa mwaka 2008, lakini akang'ara katika michuano ya vijana ya Copa Coca-Cola 2009 na 2010 iliyompa fursa ya kuitwa katika timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys'.
Atua Moro Utd
Kung'ara kwake katika kikosi cha Serengeti Boys nchini Sudan, kulitiwa Moro United, waliomsajili katika kikosi chao cha vijana 2010 ambako alifanya kweli na kuibuka mfungaji bora wa michuano ya vijana wa timu za Ligi Kuu ya Bara maarufu kama Uhai Cup kisha kupandisha hadi kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya Morogoro.
Baba yake, Mzee Hapygod Msuva, alieleza jijini hapa hivi karibuni kuwa mtoto wake huyo alisajiliwa kwa Sh. 250,000 kujiunga na Mro United akitokea kituo cha Azam FC.
Arudi Chamazi
2011 Msuva alihama Moro United na kurejea Azam FC ambako alipelekwa kikosi B na hakupewa nafasi kubwa katika kikosi cha kwanza, jambo ambalo liliushawishi ubongo wake kurejea Moro United 2012 na Yanga wakamnasa.
Anawakubali Ronaldo, Domayo
Kila mtu ana mtu anayemkubali! Msuva ni shabiki mkubwa wa mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo na kiungo wa Azam FC, Frank Domayo. Anasema anampenda Ronaldo, kutokana na aina ya uchezaji wake, lakini Domayo ni zaidi ya mchezaji na rafiki kwake.
Msuva (21) ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Yanga katika kushangilia mabao, pia ni shabiki wa Manchester United ya England.
Elimu ya darasani
Mkali huyo wa mabao alizaliwa Oktoba 2, 1993 na kusoma shule ya msingi ya Lions iliyopo Magomeni, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Atakiwa Simba
Mwishoni mwa mwaka jana, uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, ulituma maombi ambayo hayakuwa rasmi kwa uongozi wa Yanga ukitaka kumsajili Msuva.
Jambo hilo lilionekana kuwakera baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakitaka kumdunda nyota huyo kwa madai ya kucheza kinazi dhidi ya Simba katika mechi wanazofungwa na watani wao hao wa jadi.
Rekodi za wafungaji hatari VPL
Cisse Aadan alifunga mabao 19 (sawa na John Bocco na Amissi Tambwe) na kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa VPL 2005.
Boniface Ambani wa Yanga (2008/9), Musa Hassan 'Mgosi' wa Simba (2009/10, Mrisho Ngasa wa Azam FC (2010/11) waliwahi kuitwaa kwa kufunga mabao 18 kila mmoja.
Msuva na Kipre Tchetche wa Azam FC wametwaa tuzo hiyo kwa kufunga mabao 17 kila mmoja. Tchetche alifanya hivyo msimu mmoja kabla ya Tambwe kuwa Mfungaji Bora.
0 comments:
Post a Comment