Ramadhani Singano ‘Messi’ (katikati) akizungumza na waandishi wa habari
Winga wa zamani wa klabu ya Simba Ramadhani Singano ‘Messi’ amesema kwa sasa anahitaji muda wa kutulia na familia yake kabla hajajua ni wapi ataelekea kwa ajili ya kuendelea kucheza soka, jana kamati ya sheria, maadili na hadhi za wachezaji chini ya mwenyekiti wake Richard Sinamtwa iliuvunja mkataba kati ya Simba na mchezaji huyo kufuatia klabu ya Simba kutofuata masharti ya vipengele vya mkataba wao.
Messi amesema mpaka sasa hivi bado hajajua ni wapi ataelekea kwani muda mwingi alikuwa anafikiria suala lakela mkataba kati yake na klabu yake ya zamani (Simba SC).
“Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu kwa matokeo yaliyotolewa na TFF na kamati yake kwa ujumla lakini pia sina budi kuwashukuru waandishi wa habari kwa kunisapoti tena sana na pale nilipokosea naomba mnisamehe”, Messi alisema.
“Kikubwa nilikuwa nasubiri suala langu hili la kimkataba na Simba liishe maana akili yangu yote ilikuwa inafikiria suala hili na nilikua sifikirii suala jingine lolote. Sijajua nitaelekea wapi maana muda wa usajili bado upo, bado nataka nikae na familia yangu niwasikilize baba zangu, kaka zangu na washauri wangu, kwa hiyo mpaka muda huu bado sijajua chochote”, aliongeza.
“Mimi siwezi kuusemea moyo wa mtu lakini mimi bado nawakumbuka (Simba) tena sana na nimeshasahau kwa yote yale ambayo tumefanyiana kwa mazuri na mabaya na naomba pia kama kuna ubaya wowote ambao nimeufanya basi wanisamehe ten sana”, Messi aliomba radhi.
Maamuzi ya kuuvunja mkataba yaliyofanywa jana na kamati ya sheria , maadili na hadhi za wachezaji yanamfanya Messi kuwa mchezaji huru na anaweza kusajiliwa na klabu yoyote ile ambayo atakubaliana nayo.
0 comments:
Post a Comment