KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Deus Kaseke, amesema kuwa iwapo Simba itafanikiwa kuinasa saini ya straika wa Gor Mahia ya Kenya, Michael Olunga, itakuwa imelamba dume kwani ataziba pengo la Mganda, Emmanuel Okwi aliyetimkia Sonderjyske ya Denmark.
Kaseke aliyasema hayo alipozungumza na BINGWA juzi ambapo alidai kuwa Olunga ni moja ya wachezaji walioonyesha kiwango kikubwa katika mchezo dhidi yao Jumamosi iliyopita, akiwa na sifa zinazofanana na Okwi awapo uwanjani.
Alisema kama kweli taarifa zinazozungumzwa juu ya Simba kumtaka mshambuliaji huyo zina ukweli, wakifanikiwa kumsajili Wekundu wa Msimbazi hao watamsahau Okwi.
Kaseke ambaye tayari amefanikiwa kuwateka mashabiki wa Yanga kutokana na vitu vyake uwanjani, alisema: “Sio siri hivi sasa Simba inaonekana wazi inahitaji mchezaji mbadala wa Okwi ambaye alikuwa tishio kwa timu pinzani, sasa wakimpata yule mchezaji wa Gor Mahia aliyetufunga bao la pili, watakuwa wamelamba dume.”
0 comments:
Post a Comment