Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki
wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya shughuli za
sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015 hadi tarehe
24/07/2016.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015 akiwa katika onyesho
lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo
akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili. Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba,
2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza
bila kuzingatia utu na maadili awapo
jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo yake kwa nini asichukuliwe
hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha
kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba
alikiuka maadili ya kazi ya sanaa kwenye
onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria,
Kanuni na
Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.
Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa sheria na kanuni za
uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la Taifa chini ya
Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005
limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja
tokea tarehe 24/07/2015.
Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki kwa namna yoyote ile
shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi. Iwapo atafanya
kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule
utakaye shirikiana naye.
Ni matumaini ya Baraza la
Sanaa la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea
kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Sanaa ni kazi, tuipende na
kuithamini
Godfrey
Mngereza
KATIBU MTENDAJI
0 comments:
Post a Comment