Na Bertha Lumala, Dar es Salam
MSHAMBULIAJI wa Gor Mahia anayewaniwa na klabu za Azam, Simba na Yanga, Michael Olunga, amefikisha mabao manne katika michuano ya Kombe la Kagame 2015 baada ya leo alasiri kuiongoza timu yake kuifumua Telecom mabao 3-1.
Mechi hiyo ya mwisho ya Kundi A imechezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 8:00 alasiri na kushuhudia timu hiyo ya Djibouti ikimaliza hatua ya makundi bila pointi hata moja.
Gor Mahia wamepata bao la kwanza katika dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji wao George Odhiambo ambaye amekokota mpira kutoka katikati ya uwanja hadi ndani ya boksi akiwalamba chenga za fedheha mabeki wa Telecom kabla ya kupiga shuti kali la mguu wa kulia kimo cha panya lililompita kipa Nzokira Jeef aliyedaka mechi zote za Kundi A.
Mshambuliaji hatari wa Gor Mahia, Olunga, ameifungia timu yake bao la pili katika dakika ya 28 akimalizia kwa shuti mtoto la guu lake la kushoto krosi murua iliyopenyezwa ndani ya sita na winga Ronald Omino kutoka wingi ya kulia kusini mwa Uwanja wa Taifa.
Telecom waliamka kipindi cha pili na kupata bao kupitia kwa mshambuliaji mtokeabenchi Said Hassan aliyemalizia kwa kichwa mpira wa krosi uliotua ndani ya boksi kutoka kwa mtokeabenchini mwenzake Mohamed Moustafa dakika 14 baada ya saa ya mchezo.
Baada ya kuona presha ya kusawazishiwa inazidi, Gor walifanya shambuliazi la kushtukiza na kufanikiwa kufunga bao la tatu kupitia kwa straika wao Enock Angwanda aliyemchambua kwa shuti la mguu wa kulia kipa Jeef baada ya kuuwahi mpira uliotua ndani ya boksi kutoka katikati ya uwanja katika dakika ya 79.
Matokeo hayo yalmewafanya Gor wamalize mechi zote nne za Kundi A wakiwa wameshinda nne baada ya kushinda pia 2-1 dhidi ya Yanga na 3-1 dhidi ya KMKM na sare moja ya 1-1 dhuidi ya Al Khartoum ya Sudan.
Telecom pia ilifungwa 1-0 dhidi ya KMKM, 5-0 dhidi ya Khartoum na 3-0 dhidi ya Yanga.
Kikosi cha Gor Mahia kilichoanza leo kilikuwa:
Jerim Onyango, Ernest Wendo, Dirkir Glay, Eric Ochieng, Ali Abondo, Collins Okoth, Michael Olunga, Innocent Wafula, George Odhiambo, Enock Agwanda na Ronald Omino.
0 comments:
Post a Comment