Innocent Wafula (kushoto) akiwa amekumbatiana na Michael Olunga baada ya kuifungia Gor Mahia goli la pili kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Khartoum
Timu ya Gor Mahia ya Kenya imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza mchezo wa fainali ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2015 baada ya kuilaza timu Khartoum National Club kwa goli 3-1 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa leo saa 7:30 mchana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Gor Mahia wakiwa wanacheza kushangilia goli lao la pili lililofungwa na Innocent Wafula kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kagame
Khartoum ndio walikuwa wakwanza kupata bao mwanzoni mwa kipindi cha kwanza mfungaji akiwa ni Amin Ibrahim Elmani akitumia makosa ya walinzi wa Gor Mahia waliojichanya na wakidhani alikuwa kwenye nafasi ya kuotea. Baada ya goli hilo, Gor Mahia walijipanga na kufanya mashambulizi kadha na kufanikiwa kupata goli la kusawazisha kupitia kwa Michael Olunga aliyefunga kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi wa Khartoum kuunawa mpira akiwa katika harakati za kuokoa mpira langoni mwao.
Mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya Michael Olunga akijaribu kuchukua mpira mbele ya mlinzi wa Khartoum
Dakika chache badae Innocent Wafula akaifungia Gor Mahia goli la pili akiachia shuti kali lililomshinda golikipa Mohamed Ibrahim Abdalla na kutinga moja kwa moja wavuni. Kipindi cha kwanza kikamalizika Gor Mahia wakiwa mbele kwa goli 2-1.
Kipindi cha pili kilipoanza Gor Mahia hawakufanya makosa kwani dakika za mwanzo kabisa wakapiga goli la tatu lililofungwa na Kagere Medie na kuhakikishia Gor Mahia kucheza fainali ya Kagame kwa mwaka 2015 inayotarajiwa kupigwa Agosti 2 siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment