Kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa (katikati) akiongea na waandishi wa habari leo.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaondoka nchini leo jioni kuelekea Kampala - Uganda kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano dhidi ya The Cranes siku ya jumamosi.
Kikosi cha Taifa Stars kinaondoka kikiwa na wachezaji 20, bechi la ufundi 7, pamoja na viongozi, kwa shirika la ndege la Rwanda (Rwada Air) ambapo wanatarajiwa kuwasili uwanja wa Entebe majira ya saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Mchezo huo wa Jumamosi ni wa marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Rwanda, huku mechi hiyo ikichezwa saa 10 jioni katika uwanja wa Nakivubo.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema vijana wake wamefanya mazoezi vizuri katika kipindi chote cha maandalizi, na sasa wako tayari kwa mchezo huo, mipango ikiwa ni kupata ushindi siku ya Jumamosi.
Aidha Mkwasa amesema Stars itawakosa wachezaji wawili, Abdi Banda na Mohamed Hussein (Tshabalala) waliopata majeruhi jana wakati wa mazoezi yaliyofanyika uwanja wa Boko Vatereani, na kusema nafasi zao zitazibwa na wachezaji waliopo kambini.
Wachezaji wanaosafiri ni: Ally Mustafa, Mudathir Khamis, Juma Abdul, Shomari Kapombe, Haji Mngwali, Michael Aidani, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Frank Domayo, Mudathir Yahya, Salum Telela, Said Ndemla, Saimon Msuva, Deus Kaseke, Ramadhan Singano, Atupele Green, Rashid Mandawa, John Bocco na Ame Ally.
0 comments:
Post a Comment