Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Kocha mkuu wa Gor Mahia, Frank Nutall, amesema bahati imeiokoa timu yake kulala kwa kipigo kinene dhidi ya Al Khartoum katika mechi yao ya leo ya Kundi A la michuano ya Kombe la Kagame.
Mabingwa hao wa Kenya wamelazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya wawakilishi hao wa Sudan katika Kombe la Kagame mwaka huu, Gor wakisawazisha kupitia kwa kiungo wao Erick Ochieng dakika ya 42 baada ya matajiri hao wa Sudan kutangulia kupata bao dakika ya saba tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao Ousmaila Baba.
Khartoum FC walitengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini walikuwa na kiwango cha chini katika umaliziaji dhidi ya Gor ambao walikuwa imara na waliwadhibiti ipasavyo, ingawa kiwango cha leo kilikuwa si cha juu kulinganishwa na mechi mbili zilizopita walizoshinda 2-1 dhidi ya Yanga na 3-1 dhidi ya KMKM.
Nutall hajasita kuweka wazi kwamba timu yake imeshindwa kung'ara dhidi ya Wasudan hao.
"Kiwango cha wapinzani wetu kilikuwa kizuri kuzidi cha kwetu, walistahili kushinda mechi dhidi yetu kwa sababu wachezaji wao walionekana kutaka ushindi kuliko wachezaji wetu. Na kama tungeshinda, ungekuwa ushindi tusiostahili," amesema kocha huyo baada ya mechi.
Timu zote mbili ziko Kundi zikiowa kileleni mwa msimamo baada ya kukusanya pointi saba kila moja, lakini Khartoum iko juu kwa tofauti ya magoli (+6).
Gor itafunga hatua ya makundi kwa kuikabili timu kibonde katika Kundi A, Telecom wakati Khartoum itakuwa na mtihani mgumu mbele ya wenyeji Yanga Jumapili.
0 comments:
Post a Comment