Kocha wa Gor Mahia Frank Nuttal leo ameongoza mazoezi ya kikosi chake kwenye uwanja wa Karume katika mfululizo wa kukiweka sawa kikosi hicho kwa ajili ya michuano ya Kagame inayoendelea kupamba moto jijini Dar es Salaam.
Licha ya timu yake kuwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo, Nuttal amesema bado anahitaji ushindi kwenye michezo iliyosalia kwenye kundi lake ili kuendelea kutengeneza historia ya kutopoteza mechi lakini pia kuzidi kuweka heshima kwenye michuano hiyo.
“Timu yangu imefuzu kucheza hatua ya robo fainali, lakini hiyo hatufanyi kudharau mechi zetu zilizobaki kwenye kundi. Tunahitaji kushinda michezo hiyo ili kuendeleza rekodi yetu ya kutopoteza mchezo lakini tunataka kuweka heshima kwenye mashindano haya”, amesema.
“Tumecheza michezo 18 bila kupoteza kwenye ligi ya Kenya, hapa tumeshinda mechi mbili halafu bado tuna michezo mingine miwili kwenye kundi letu ambayo tunatakiwa kushinda. Mashindano ni magumu ndio maana utaona hata sisi tumeruhusu magoli japo tumekuwa tukipata ushindi”, amefafanua.
“Kwenye mechi zijazo nitawapa nafasi wachezaji ambao bado hawajapata nafasi ya kucheza kwenye mechi zilizotangulia”, alimaliza.
Wachezaji waliofanya mazoezi leo ni wale ambao hawakucheza kwenye mchezo wa jana wakati Gor Mahia ilipoibuka na ushindi wa goli 3-1 dhidi ya KMKM mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa. Gor Mahia mpaka sasa ndio inaongoza ligi ya Kenya ikiwa bado haijapoteza hata mchezo mmoja lakini ikiwa imeruhusu magoli nane tu kwenye mechi 18.
0 comments:
Post a Comment