Timu ya Azam FC ‘wanalambalamba’ leo wametoa dozi ya magoli 5-0 kwa Adama City FC ya Ethiopia kwenye mashindano ya Kagame Cup ambayo yanazidi kuchanja mbuga jijini Dar es Samaa mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Kipre Tchethe amefunga magoli mawili kwenye mchezo wa leo, Kipre alianza kufunga goli la kwanza dakika ya nane kipindi cha kwanza, Tchetche tena akarudi kambani kufunga goli la pili kwa upande wa Azam dakika ya 19 ya mchezo.
Shah Farid Mussa akaiandikia Azam goli la tatu dakika ya 35 kipindi cha kwanza akiunganisha pasi safi kutoka kwa Erasto Nyoni. Kipindi cha kwanza kilimalizika Azam wakiwa mbele kwa magoli 5-0.
Kipindi cha pili Azam walirejea uwanjani wakiwa bado wana njaa ya magoli kwani dakika nne baada ya kipindi cha pili kuanza, Mudathir Yahya aliifungia Azam goli la nne.
Dakika ya 79 Agrey Morris alifunga goli la tano kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi wa Adama City Moges Tadese kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Wachezaji wa Adama City walijikuta wakimaliza mpira wakiwa tisa kufutia wachezaji wao wawili kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Wachezaji waliotolewa kwa kadi nyekundu kwa upande wa Adama City ni Eshetu Menna na Moges Tedese.
Azam walifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwatoa Kipre Tchetche na nafasi yake ikachukuliwa na Didier Kavumbagu wakati Said Morad aliingia kuchukua nafasi ya Pascal Wawa na Agrey Morris akapumzishwa kumpisha Kamagi Gadiel Michael.
Mchezo wa kwanza uliopigwa majira ya saa 8:00 mchana ulikuwa ni kati ya KCCA ya Uganda dhidi ya Malakia FC ya Sudan Kusini na mchezo huo ukamalizika kwa KCCA kuibuka na ushindi wa goli 1-0.
Kesho michuano hiyo itaendelea tena kwenye uwanja wa Taifa ambapo timu za kutoka Kundi A zitakuwa vitani, mchezo utakaoanza saa 8:00 mchana utakuwa ni kati ya Gor Mahia ya Kenya dhidi ya Telecom ya Djibouti wakati mchezo wa saa 10:00 jioni utakuwa ni kati ya Yanga dhidi ya Khartoum National Club ya Sudan.
0 comments:
Post a Comment