Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
NYOTA mahiri na maarufu katika ukanda wa CECAFA, Jean-Baptiste Mugiraneza na mshambuliaji hatari wa El-Merreik Allan Wanga wamesajiliwa Azam FC, mabingwa hao wa Tanzania Bara 2013/14 wamethibitisha.
Mugiraneza mwenye uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi na kiungo, alikuwa anaitumikia klabu ya 'maafande wa Rwanda, APR wakati Wanga amemaliza mkataba wake na El-Merreikh.
Wanga raia wa Kenya, ndiye aliyeing'oa Azam FC katika michuano ya Klabu Bingwa mwaka huu akifunga bao la mwisho wakati El-Merreikh ikiwashindilia 'Wanalambalamba' mabao 3-0 mjini Khartoum mwanzoni mwa mwaka huu.
Mtandao rasmi wa klabu ya Azam FC umeripoti kuwa mazungumzo na Wanga yamefika sehemu nzuri wakati Mugiraneza ambaye tayari ameichezea Azam mechi mbili za kirafiki dhidi ya Africans Sports na Coastal Union, atasajiliwa lakini ataitumikia APR katika michuano ya Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam kabla ya kujiunga na kikosi cha Muingereza Stewart Hall moja kwa moja.
Uongozi wa Azam FC umeeleza kuwa Wanga amekuwa kwenye rada zao kwa muda mrefu tangu alipofunga goli lililoisaidia Merreikh kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mjini Kigali, Rwanda mwaka jana.
BIDVEST
Mtandao wa habari za michezo wa Futaa.com wa Kenya, ulisema jana kuwa Wanga, mshambuliaji hatari wa timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars', wiki iliyopita alikuwa na mazungumzo ya kusajiliwa na klabu ya Bidvest Wits ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), lakini tayari alikuwa amweshafikia makubaliano na Azam FC.
Usajili wa nyota hao wawili Chamazi unafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa Azam FC msimu huu kufika wanne. Wengine ni wazalendo Ame Ally Amour kutoka Mtibwa Sugar na Ramadhan Singano 'Messi' aliyeikacha Simba baada ya kutangazwa kuwa ni mchezaji huru na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
0 comments:
Post a Comment