Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
HUKU Hans van der Pluijm dhidi ya Ali Bushir, kule Stewart Hall dhidi ya Felix Minziro! Ndivyo unavyoweza kusema katika mechi za kirafiki za kesho jijini hapa.
Wakati Yanga watakuwa wenyeji wa KMKM katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, JKT Ruvu watakuwa wageni wa Azam FC katika mechi nyingine ya kesho ya kirafiki Uwanja wa Azam jijini hapa.
Kocha mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall, amekaririwa katika mtandao rasmi wa klabu hiyo leo akieleza kuwa ataitumia mechi ya leo kuwapima wachezaji wake akiwamo kipa Muivory Coast Vincent Atchouailou de Paul Angban.
Vincent alitua Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na leo atacheza mchezo huo wa kwanza kwenye kikosi cha Azam ambacho kitakuwa na mtihani mgumu kuwazuia washambuliaji wapya wa kikosi cha kocha mkuu mzawa Felix Minziro cha JKT Ruvu; Saad Kipanga, Amour Omary Janja na Gaudence Mwaikimba ambaye alikipiga katika kikosi cha Wanalambalamba msimu uliopita.
"Tunaendelea vizuri na mazoezi na Jumanne (kesho) tutacheza mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu kwa ajili ya kujipima. Katika mchezo huo ninatarajia kumtumia kipa Muivory Coast aliyewasili wikiendi hii kwa majaribio," amesema Hall.
Mechi hiyo ni ya pili kwa Azam tangu kurejeshwa kwa mara ya pili kwa kocha huyo Mzungu baada ya wiki iliyopita kuifunga Friends Rangers mabao 4-2 jijini.
Azam FC inajiandaa kwa michuano ya Kombe la Kagame itakayofanyika jijini kuanzia Julai 18.
0 comments:
Post a Comment