Azam FC ndio wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia kwenye michuano ya Kagame Cup licha ya Tanzania kuwakilishwa na timu tatu kwenye michuano hiyo. Yanga, na Azam zilikuwa zikiiwakilisha Tanzania bara wakati KMKM ilikuwa ikiwakilisha visiwa vya Zanzibar lakini tayari Yanga na KMKM zimesha yaaga mashindano hayo na kuicha Azam pekee ikiiwakilisha Tanzania.
Leo Azam inacheza mchezo wa nusu fainali ya Kagame kwa mwaka 2015 ikikutana na timu ya KCCA ya Uganda kwenye mchezo ambao utaamua ni timu gani kati ya hizo itaingia fainali ya mashindano hayo kwa mwaka huu.
Mpaka sasahivi Azam haijaruhusu wavu wake kutikiswa na timu yoyote ndani ya dakika 90, hii imekuwa timu pekee kwenye mashindano ya mwaka huu kuingia kwenye hatua ya nusu fainali ikiwa haijafungwa goli hata moja mpaka sasa na kujiwekea rekodi kwenye michuano hii. Lakiki kwa upande mwingine Azam inaungana na Gor Mahia kuwa timu mbili pekee ambazo zimeingia kwenye nusu fainali zikiwa hazijapoteza mchezo hata mmoja tangu ngazi ya makundi.
Azam iliyoiondosha Yanga kwenye michuano hii zilipokutana kwenye hatua ya robo fainali na kuitupa timu hiyo nje ya mashindano kwa changamoto ya mikwaju ya penati 5-3 imefanikiwa kufunga magoli tisa mpaka sasa ikianza kwa kuifunga KCCA goli 1-0, ikapata ushindi mwingine wa goli 3-0 dhidi ya Malakia FC kisha kuifumua Adama City kwa goli 5-0 na kutinga hatua ya robo fainali na kuitoa Yanga kwa penati.
Azam ilikuwa kundi moja na KCCA ya Uganda zote zikiwa zimepangwa kundi C na Azam walishinda mchezo wao dhidi ya KCCA kwa goli 1-0 goli lililofungwa na John Bocco ‘Adebayor’. Hivyo mchezo wa leo utakuwa ni wa kisasi au ubabe, KCCA wakitaka kulipa kisasi kwa kuifunga Azam iliyowafunga kwenye mchezo wa kwanza wakati Azam itakuwa inataka kuendeleza ubabe wa kuifunga tena KCCA.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum ambazo pia zilikuwa kwenye kundi moja la A na timu hizo zilipokutana zilitoka sare ya kufungana kwa goli 1-1. Gor Mahia haijapoteza mchezo hadi sasa, imefika nusu fainali kwa kuisukuma nje ya mashindano timu ya Malakia kwa kuifunga goli 2-1 kwenye mchezo wa robo fainali. Khartoum yenyewe imepoteza mchezo mmoja ambapo ilifungwa na Yanga kwa goli 1-0 kwenye hatua ya makundi.
Khartoum imetinga hatua ya nusu fainali kwa kuiondosha timu ngumu na kongwe kwenye michuano ya Kagame APR FC ya Rwanda kwa kuipa kichapo cha mbwa mwizi kwa kuibugiza goli 4-0 na kuwa timu ambayo imefunga magoli mengi hadi sasa ikiwa imefunga magoli 12. Mechi ya kwanza ilianza kwa ushindi wa goli 5-0 mbele ya Adana City, 2-1 dhidi ya KMKM, 1-1 dhidi ya Gor Mahia na 4-0 ilipochuana na APR.
Mchezo kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na walimu wote kutumia mbinu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa matokeo wanayo yataka. Kwesi Appiah kocha wa Khartoum amekuwa na mbinu nyingi sana za kupata matokeo licha ya timu yake kuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya.
Ni kocha mwenye uzoefu wa hali ya juu na ameshakutana na mechi kubwa na ngumu nyingi kuliko ilivyo kwa Kagame.Wakati kocha wa Gor Mahia Frank Nuttal anajivunia rekodi yake ya kutopoteza mcheo na Gor Mahia.
0 comments:
Post a Comment