Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
RAIS wa Simba, Evans Aveva, amesema mshambuliaji aliyetemwa Yanga, Hamis Kiiza atawasili nchini wakati wowote na kpimwa afya kabloa ya kusaini mkataba kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi.
Aveva, aliyekuwa amefuatana na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu' katika hafla ya uzinduzi wa kadi ya watoto ya uanachama wa Simba jijini hapa leo mchana, amesema wamefikia hatua nzuri na mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya URA ya Uganda.
"Mazungumzo yetu na Kiiza yamekwenda vizuri, muda wowote kuanzia leo (jana) atawasili nchini kwa ajili ya kupimwa afya. Akifuzu vipimo vya afya, tutamsajili kuwa miongoni mwa wachezaji wetu," amesema Aveva.
Ingawa kiongozi huyo wa juu wa Simba hakutaja muda wa mkataba ambao Kiiza atasaini, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope amesema leo kuwa nyota huyo atatia saini ya kandarasi ya miaka miwili.
“Sisi na Kiiza kila kitu safi, anakuja kusaini miaka miwili hapa,” ametamba Hanspope.
Kiiza aliachwa na Yanga Desemba mwaka jana ili kumpisha mshambuliaji Mliberia Kpah Sherman baada ya kuitumikia klabu hiyo tangu 2011.
Tangu atemwe na mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara, Mganda huyo anayetisha kwa kupachika mabao, amekaa bila timu baada ya mpango wake wa kwenda kucheza Fanja ya Oman kushindikana Januari mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment