MABINGWA wa Kandanda Tanzania bara, Young Africans asubuhi
hii wanaanza mazoezi kujiandaa na ligi kuu soka Tanzania bara pamoja na
michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati, Maarufu kama Kombe la Kagame
inayotarajia kuanza kutimua vumbi Julai 11 mwaka huu.
Kocha mkuu wa Yanga aliyerejea nchini usiku wa kuamkia jana,
Hans van der Pluijm analazimika kuanza mazoezi mdogo-mdogo na wachezaji
wachache kwani wengi wapo timu zao za Taifa.
Pluijm anaanza kuwanoa vijana wake leo uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, Dar es salaam na kufikia Juni 16 mwaka huu wachezaji wote watakuwa
wameripoti, ingawa Kpah Sherman raia wa Liberia anatua leo nchini.
Wakati huo huo, Yanga inasubiri Baraka za TFF kuhusu idadi
ya wachezaji 10 wa Kigeni aliopendekeza wasajiliwe kuelekea msimu ujao, lakini
tayari imeeleza kwamba ina majina yote ya wanandinga inaowataka.
“Wachezaji wa Kigeni tumeshawapata, tunachosubiri ni TFF
kutangaza idadi tunayoruhusiwa kusajili. Tuliomba idadi iongezwe kutoka watano
wa sasa mpaka kufikia 10, wakitoa Baraka zao, basi tutatangaza wachezaji
tuliozungumza nao na imebaki kuwasainisha tu”. Amesema katibu mkuu wa Yanga,
Dr. Jonas Tiboroha.
0 comments:
Post a Comment