Na Ramadhani Ngoda
Miaka 19 ya Mfaransa
Arsene Wenger katika klabu ya Arsenal ni sawa na ‘chungu tamu’ maana ina
mazuri na mabaya ya kuhadithia kwa wapenzi wa klabu hiyo yenye maskani yake
Kaskazini mwa jiji la London.
Tangu kuwasili kwake
Higbury (wakati huo) mnamo mwaka 1996, ni wazi kuwa amefanya makubwa
yanayostahili chungu ya shukrani kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo. Moja ikiwa
ni kuipa Arsenal mataji matatu ya ligi kuu mpaka sasa akifuta ukame wa miaka 7
bila taji la ligi kwani taji la mwisho kwa Arsenal lilikuwa ni msimu wa 1990/91
chini ya George Graham kabla ya Wenger kurudisha heshima hiyo msimu wa 1997/98
na kushinda mengine miaka ya 2002 na lile la 2003/04.
Arsenal akishangilia ubingwa wa ligi kuu Uingereza msimu wa 1997/98 |
Ni kweli walivyonena
waswahili, ‘mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.’ Kubwa jingine linaloweza
kuwa dhahabu ya Wenger kwa wana Arsenal, ni mataji 6 ya kombe la FA chini ya uongozi
wake katika klabu hiyo. Ikumbukwe kuwa hakuna kocha aliyewahi kuchukua hata
mataji mawili ya kombe hilo tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka 129 iliyopita
kuanzia Thomas Mitchell hadi Pat Rice aliyekabidhi kijiti kwa Wenger. Hongera
‘profesa’ kwa hili.
Lakini kama hiyo
haitoshi, Arsenal watakumbuka medali za mshindi wa pili walizovaa mwaka 2006
japo waliusaliti ubingwa huo kwa wababe wa Hispania FC Barcelona. Fainali
iliyodhihirisha kweli ‘la kuvunda halina ubani’ kwani ilikuwa ni nafasi pekee
ya Arsenal kutwaa kwa mara ya kwanza taji hilo kutokana na ukweli kuwa
mashabiki, wachezaji pamoja na makocha waliowahi kuinoa Arsenal, hawajui ladha
ya taji hilo kubwa barani barani Ulaya. Lakini kwa walichoambulia si haba.
‘Utamu wa muwa ni
fundo.’ Mzee Wenger ni lazima akiri kuwa ana madeni kwa wana Arsenal ambayo
pengine kuyalipa kabla hajajafikia ukomo wa maisha yake Emirates ni jambo bora
na la kihistoria litakalomfanya akumbukwe Zaidi klabuni hapo.
Kubwa la madeni mengi
aliyonayo, ni kuipa Arsenal kitu wanachokishuhudia tu kwa vilabu vingine kama
FC Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Manchester United, Liverpool na
nyingine nyingi barani Ulaya. Na hili si jingine bali ni Ligi ya mabingwa
barani Ulaya.
Arsene Wenger baada ya fainali ya ligi ya mabingwa msimu wa 2005/06 dhidi ya FC Barcelona na kuambulia nafasi ya pili |
Kuhama kutoka uwanja
wa zamani wa Highbury kwenda Emirates, kumekuwa kukitajwa kama kichocheo
kikubwa cha Arsenal kushindwa kusajili wachezaji wenye majina makubwa kama
tunavyowaona sasa na wengine wakizidi kutajwa. Hii ni ishara kuwa, sasa mzee
Wenger atakuwa hana kisingizio kwani anapewa donge kubwa la usajili ili kujenga
kikosi chenye ushindani kitakacholeta ‘champions league’ katika uwanja wa
Emirates.
Alexis Sanchez, Mesut
Ozil, David Ospina na Mathew Debuchy wanaonekana kuwa mwanzo tu wa ujio wa
majina mengi makubwa katika klabu hiyo kama walivyokwisha taja wakiana Arturo
Vidal, Morgan Schdeiderlin, Edinson na wengine. Lipo linalotafutwa bila shaka.
Wenger lipa deni hili kwa watu waliokuvumilia kwa Zaidi ya miaka 10
uliyoboronga.
Deni la pili linaweza
kuwa taji la ligi kuu nchini humo ambalo licha ya kuvunja ukame wake mwaka 1998
(mwaka wa pili baada ya kuichukue Arsenal), taji hilo limekuwa adimu Zaidi ya
nyota ya jaha kwa wapenzi wa klabu hiyo kwani hawajaliona sura yake tangu mwaka
2004 walipochukua kwa mara ya mwisho.
Ukiacha ukweli kuwa,
taji la FA walilotwaa msimu wa 2013/14, ni taji lililofuta vumbi kabati la
mataji ya klabu hiyo kwa miaka 10, bado wanazi hao wana kiu ya miaka 11 ya taji
la ligi kuu nchini humo. Bila shaka wanaumia na kuchoshwa na kuziona Manchester
city, Manchester United na Chelsea wakipokezana ubingwa huo kama mbio za
vijiti. Wenger inambidi kutengeneza chemchem ya maji itakayokata kiu hii ya
Zaidi ya muongo mmoja sasa.
Bila shaka anatakiwa
kwa namna moja au nyingine kutilia maanani maneno ya wakongwe wa klabu hiyo,
wakina Robert Pires, Patrick Vieira, Rey
Parlour na wengine waliowahi kumshauri aongeze wachezaji wenye uwezo mkubwa
wanaoweza kushindana ndani ya Uingereza lakini pia barani Ulaya. Bila shaka
hawa walitaka kuwaona wakina Sanchez na Ozil wengi wakisajiliwa Arsenal. Na
hili ndio linaloonekana kuwa katika akili za wana Arsenal wengi duniani kote.
0 comments:
Post a Comment