Tuesday, June 16, 2015

'Wachambuzi wengi wa soka waliokosoa tuzo za TPLB wameinyooshea kidole bodi hiyo hata katika vipengele ambavyo imetenda haki kutoa tuzo husika.'

 
WIKI iliyopita Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilikabidhi zawadi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2014/15 na kuwatunuku tuzo wachezaji, refa, kocha na timu zilizofanya vyema.

Katika hafla ya tuzo hizo iliyofanyika jijini Dar es Salaam Alhamisi usiku, winga wa Yanga aliyeibuka mfungaji bora, Simon Msuva, alitangazwa Mchezaji Bora wa msimu.

Kipa wa zamani wa Mtibwa Sugar na Yanga, Shaaban Kado alitwaa tuzo ya Kipa Bora wakati kipa wa zamani wa Yanga, Mbwana Makatta akimrithi Juma Mwambusi wa Mbeya City katika kipengele cha Kocha Bora.

Mabingwa mara mbili wa Tanzania Bara, Mtibwa Sugar walishinda tuzo ya Timu yenye Nidhamu wakati refa mzoefu Israel Nkongo wa Dar es Salaam akiibuka mshindi wa tuzo ya Mwamuzi Bora wa msimu.

Kumeibuka minong'ono mingi baada ya kutolewa kwa tuzo hizo huku baadhi ya makocha na viongozi wa klabu za soka nchini wakiponda tuzo za baadhi ya vipengele.

NIPASHE Viwanjani inayofuatilia kwa kina VPL, leo inachambua tuzo hizo. Karibu...

MFUNGAJI BORA
Hii haina ubishi kwa sababu mfungaji bora ni yule aliyefunga mabao mengi zaidi katika msimu husika. Msuva alifunga mabao 17 ikiwa ni mawili pungufu ya mabao yaliyofungwa na Mfungaji Bora wa VPL msimu wa 2013/14, Mrundi Amissi Tambwe.

Msuva hakuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kilichokuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo katika raundi saba za mwanzo.

Baada ya kurejeshwa kwa Mdachi Hans van der Pluijm na msaidizi wake Boniface Mkwasa, Msuva aliaminika na kufunga mabao mengi.

Kukosekana kwake katika mechi mbili za mwisho walizolala 2-1 dhidi ya Azam FC na 1-0 dhidi ya Ndanda FC, huenda ndiko kulimnyima fursa ya kuifikia au kuipiku rekodi ya Jonh Bocco 'Adebayor' wa Azam na Tambwe kwa kufunga mabao 19 msimu mmoja.
 
MCHEZAJI BORA
Katika kipengele hiki kilichoambatana na zawadi ya Sh. milioni 5.7, beki wa kushoto Mohamed Hussein 'Tshabalala' wa Simba na winga Mrisho Ngasa aiyekuwa Yanga msimu uliopita ndiyo walioingia kuchuana na Msuva.

Kwa waliofuatilia kwa kina msimu uliopita, watakubaliana na mimi kwamba kiwango cha Ngasa, Mchezaji Bora wa VPL mwezi Aprili 2015, kilikuwa kimeshuka mzunguko wa kwanza kabla ya kurejea katika makali yake mzunguko wa pili.

Alifunga mabao manne msimu mzima wa VPL ikiwa ni mabao nane pungufu ya msimu wa 2013/14. Licha ya kutoa pasi nyingi za mabao mzunguko wa pili zikiwamo tatu katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Police Moro, Ngasa hakustahili kuingia kwenye kipengele cha Mchezaji Bora kutokana na kuzidiwa mno kitakwimu na wakali wengine.

Kwa mtazamo wngu, kiungo mshambuliaji wa Simba kutoka Uganda, Emmanuel Okwi alipaswa kuwamo katika orodha hiyo ya kumsaka Mchezaji Bora badala ya Ngasa. 

Okwi alifunga mabao 10 na alikuwa mpishi mzuri wa magoli mengi yaliyofungwa na Ibrahim Ajibu na Elias Maguri. Kila goli lililofungwa na Mganda huyo lilikuwa na maana kubwa kwa kikosi cha Mserbia Goran Kopunovic.

Kila alipofunga, Simba ilipata pointi tatu au kuambulia sare. Kumbuka magoli yake dhidi ya Yanga, Mtibwa, Prisons na Mgambo. Kwa kifupi, ukiondoa magoli yote ya Okwi, Simba itakuwa miongoni mwa timu ambazo zingeshuka daraja.

Tshabalala ni miongoni mwa wachezaji wachache waliocheza mengi nyingi zaidi msimu uliopita. Hata angeshinda tuzo hii, kusingekuwa na shaka kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha.

Akiwa ni sehemu ya ukuta wa Simba, beki huyo aliiwezesha timu yake kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa VPL na kwenye orodha ya timu zilizofungwa mabao machache zaidi. Simba ilifungwa mabao 19, moja mbele ya Yanga na Azam FC.

Tuzo ya Mchezaji Bora kutua kwa Msuva sioni tatizo kutokana na mchango wa winga huyo katika kuipa ubingwa timu yake. Mbali na kufunga mabao, mcheza shoo huyo wa zamani wa THT alipika mabao muhimu likiwamo goli la kwanza lililofungwa na Tambwe katika dakika ya 41 ya mechi yao ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Police Moro.

Msuva alifunga mabao muhimu katika mechi ambazo Yanga ilionekana kuzidiwa. Kumbuka mabao yake matatu katika mechi zote mbili dhidi ya Mgambo Shooting ambazo hata hivyo, zilifinyangwa na marefa. Zikumbuke pia mechi za Dar es Salaam dhidi ya JKT Ruvu, Kagera Sugar na Stand United.

KOCHA BORA
Hapa pana tatizo! Makatta aliiongoza Tanzania Prisons katika mechi nane akirithi mikoba ya kocha wa Simba 1999, David Mwamaja ambaye alitimuliwa baada ya timu kukaa mkiani kwa muda mrefu.

Licha ya kufanya vyema katika mechi hizo nane zikiwamo alizoshinda dhidi ya City, Coastal, Stand United na Mgambo, Makatta hakustahili hata kuingia katika orodha ya kumsaka Kocha Bora kutokana na idadi ndogo ya mechi alizoiongoza timu yake. Mechi nane hazifiki hata theluthi ya mechi zote za ligi.

Pluijm na Kopunovic walistahili kuingizwa katika orodha hiyo kwa misingi ya kitakwimu, lakini uhalisia wa soka la Tanzania unawanyima kutwaa tuzo hiyo.

Pluijm amefanya kazi kubwa kukibadili kikosi cha Yanga kufuata soka lake la kushambulia mfululizo. Mafanikio ya Yanga msimu uliopita ilikuwa sifa kuntu ya kumpa tuzo ya Kocha Bora, lakini inakuwa ngumu kupima ubora wake kutokana na timu yake kuonekana kubebwa na mamla ya soka nchini (TFF).

Shirikisho lilionekana kuibeba Yanga liliposita kuwaadhibu baadhi ya nyota wa klabu hiyo akiwamo nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na Tambwe ambao kwa nyakati tofauti walitenda makosa ya kinidhamu kwa kuwadhalilisha askari polisi mwanamke na beki wa kati wa Simba, Juuko Murshid.

Pia baadhi ya mechi za Yanga zilionekana kufinyangwa na marefa. Kadri ya uelewa wangu wa soka, marefa waliionea Mgambo katika mechi zote mbili ilizolala 2-0 Dar es Salaam na Pwani.

Miezi miwili iliyopita Mkufunzi wa Marefa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Leslei Liunda, alisema: Kama ningekuwa ninachezesha mimi mechi ya Mgambo dhidi ya Yanga, Cannavaro na Kelvin Yondani wasingemaliza 'first half' (kipindi cha kwanza) bila kuwatoa kwa kadi nyekundu."

Katika mechi ya kwanza ambayo Yanga ilishinda 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, refa Ngole Mwangole alikataa penalti halali ya Mgambo iliyotokana na kiungo mshambuliaji Malimi Busungu kukwatuliwa ndani ya boksi na beki wa pembeni kulia Juma Abdul kisha refa huyo kutoka Mbeya akaruhusu bao lisilo halali la Msuva aliyepiga shuti katika lango tupu kufuatia mshambuliaji Hamis Kiiza kumwangusha kipa wa Mgambo.

Licha ya kufanya vizuri kulinganishwa na 2013/14, Simba nao walibebwa na TFF katika baadhi ya mechi. Timu hiyo ilitumia kanuni mpya ya kadi tatu za njano ambayo ilikuwa haijazifikia klabu kwa kuwapanga kikosini Abdi Banda na Ajibu katika mechi dhidi ya Stand United, Tanzania Prisons na Yanga.

Kwa mtazamo wangu, tuzo ya Kocha Bora wa VPL 2014/15 ilipaswa kutua kwa Mwambusi kwa mara ya pili kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kuhakikisha timu hiyo haiporomoki daraja na baadaye kupambana kumaliza katika nafasi nne za juu.

Ikumbukwe kuwa City ilikaa mkiani mwa msimamo kwa muda mrefu mzunguko wa kwanza. Mwambusi pia ni miongoni mwa makocha wachache ambao waliongoza timu zao katika mechi zote 26 bila kufukuzwa au kufungiwa na TFF. Makocha wengine ni Bakari Shime wa Mgambo, Mecky Mexime wa Mtibwa, Felix Minziro wa JKT Ruvu na Tom Olaba wa Ruvu Shooting.

MWAMUZI BORA
Refa mzoefu mwenye beji ya Fifa, Israel Nkongo wa Dar es Salaam, aliwabwaga Jonesia Rukyaa na Samuel Mpenzu katika tuzo hiyo iliyokuwa na zawadi ya Sh. milioni 8.6.

Kwa wanaofuatilia kwa kina watakubaliana na mimi kwamba Nkongo anastahili tuzo hiyo kutokana na ubora aliouonesha msimu uliopita.
Nilipoandika katika safu hii miezi miwili iliyopita kuhusu makosa nane sugu ya marefa wa Tanzania, nilieleza namna Nkongo alivyokuwa mwalimu bora kwa marefa wenzake.

Nkongo anajua mahali sahihi pa kusimama kutokana na hali ya mchezo. Hakurupuki katika kutoa uamuzi. Nkongo pia alikuwa mstari wa mbele katika kuwasahihisha wenzake pale walipokosea. Suala hilo alikuwa analifanya kwa kuwafuata vyumbani baada ya mechi husika kumalizika. Suala hili halikuwahi kuripotiwa, lakini NIPASHE Viwanjani ilifuatilia na kulibaini. Hakika anastahili tuzo hiyo!

TIMU YENYE NIDHAMU
Uongozi wa Simba kupitia kwa msemaji wa klabu hiyo, Hajji Manara, uliitupia lawama TPLB kwa kuipa Mtibwa Sugar tuzo hiyo.

Katika kipengele hicho Mtibwa Sugar ilikuwa inachuana dhidi ya Mgambo JKT na Simba kusaka zawadi ya Sh. milioni 17.2.

"Sisi hatukuwa na kadi nyekundu hata moja, lakini wenzetu Mtibwa walipata kadi nyekundu mbili," alisema Manara.

Hata hivyo, takwimu za NIPASHE Viwanjani zinaonyesha kuwa Mtibwa hakuna mchezaji hata mmoja wa Mtibwa aliyeonyeshwa kadi nyekundu msimu uliopita. Timu hiyo ilipata kadi 32 za njano na inakamata nafasi ya kwanza katika orodha ya timu zilipata kadi chache.

Kwa takwimu hizo, ni wazi kwamba Simba wanatapatapa. TPLB wametenda haki katika hili. Mtibwa ilistahili tuzo ya Timu yenye Nidhamu.

Jambo pekee ambalo lingeweza kuiangusha Mtibwa katika tuzo hii ni kitendo cha mmoja wa watendaji wake kudaiwa kumtukana matusi na kumtishia maisha refa Jonesia kutokana na matokeo mabaya ya kipigo cha 2-1 katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezeshwa na refa huyo kutoka Kagera.

KIPA BORA
Timu zilizofungwa mabao machache zaidi msimu uliopita ni Yanga (18), Azam (18) na Simba (19), lakini hazikutumia kipa mmoja msimu mzima.

Simba iliwatumia makipa wake wote watatu Ivo Mapunda, Peter Manyika Jr na Hussein Sharrif 'Casillas' aliyedaka mechi mbili. Yanga iliwatumia Ali Mustafa 'Barthez' na Deogratius Munishi 'Dida' wakati Azam FC nayo ilitumia makipa wawili Aishi Manula na Mwadini Ali.

Unapofuatilia utendaji wa kipa mmoja mmoja, Mohamed Yusuph wa Prisons, Shaaban Kado, Said Mohamed 'Nduda' na Aishi Manula wanaingia katika orodha ya makipa waliofanya vyema msimu uliopita.

Hata hivyo, utovu wa nidhamu unamwondoa Manula katika orodha ya kupata tuzo ya Kipa Bora kwani kigezo hicho kilizingatiwa na TPLB. Katika mechi ya Kagera dhidi ya Azam FC jijini Mwanza, kipa huyo aliripotiwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa kumtukana mmoja wa marefa wa mechi hiyo.

NIPASHE Viwanjani ilidokezwa na mmoja wa watendaji wa TPLB kwamba tukio hilo liliripotiwa na marefa wa mechi hiyo, lakini kipa huyo hajachukuliwa hatua na TFF.

Licha ya kuibuka msuguano katika kikosi cha mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union kulikosababisha kuwa nje ya kikosi katika mechi za mwishoni mwa msimu, Kado alifanya kazi nzuri katika mechi alizokuwa langoni.

Yusuph na Nduda walifanya kazi nzuri, lakini takwimu za timu zao zinawaangusha wanapopambanishwa na Kado. Coastal Union ilifungwa mabao 25, Mtibwa ilifungwa mabao 26 wakati Prisons ilifungwa mabao 22.

Kipigo kibaya cha mabao 8-0 dhidi ya Yanga ndicho kiliifanya Coastal kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufungwa, lakini Kado hakudaka katika mechio hiyo.

Katika mechi 19 za mwanzo ambazo Kado alikuwa langoni, Coastal ilifungwa mabao 13. Kwa takwimu hizi, ni wazi kwamba TPLB haijakosea kumpa tuzo ya Kipa Bora wa msimu.


*Imeandikiwa na Sanula Athanas ambaye ni mwandishi wa michezo mwandamizi wa NIPASHE. Pia ni mshindi wa tuzo ya Mwandishi Bora wa Habari za Michezo na Utamaduni Tanzania Mwaka 2014. 

CHANZO: GAZETI LA NIPASHE la Jumnatatu Juni 15, 2015

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video