Wakati chama cha kutetea wachezaji Tanzania (SPUTANZA) kikiendelea na sakata la kimkataba la mchezaji Ramadhani Singano ‘Messi’ na klabu yake ya Simba, wadau wa soka wamejitokeza na kukipigia kelele chama hicho kwa kudai chama hicho kinatetea haki za wachezaji wa sasa pekee na kusahau wachezaji wa miaka iliyopita.
Aliyewahi kuwa kiungo wa Simba wakati huo ikijulikana kwa jina la Sunderland, Hamisi Kilomoni mesema, chama hicho kimepoteza uasili wake kwa kujigeuza kuwa chama cha wachezaji wa sasa licha ya kazi nzuri inayofanywa na chama hicho.
Kilomoni amesema ni wakati sasa kwa viongozi wa chama hicho kujirejesha katika uasisi wake kwa lengo la kuwasaidia pia hata wachezaji wa zamani.
“SPUTANZA wasibague, wanabagua wachezaji wa mwaka huu mpaka wa mwaka huu, siyo kazi yao, kazi yao ni kuona kwamba wachezaji wa Tanzania hii wanapata haki zao wanazostahili, hiyo ndiyo kazi yao”, amefafanua.
“Hii SPUTANZA haikuanzishwa na wachezaji wa sasa, ‘originally’ hii SPUTANZA ilianzishwa na wachezaji wa zamani lakini hapo katikati ilitaka kufa kwasababu kuna watu juu huko walikuwa hawataki hiyo kitu iendelee, lakini naona vijana wa sasahivi wamejitahidi mpaka wameifanya iko kwenye dhamana ya michezo lakini mwanzoni mwa SPUTANZA sio kama ilikoanzia,” amesema Kilomoni.
“Hata kama mimi ningetaka ningekuwepo SPUTANZA, tulianza hivyohivyo matatizo yaliyokuwepo SPUTANZA ni ile kupata msukumo maana tulipoanzisha wenzetu wa serikali walikuwa hawataki. Hii ilituletea ugumu kidogo, kuna watu walikuwa wanataka wengine hawataki, ilituletea ugumu mpaka sisi wengine tukaamua kukaa pembeni,” ameongeza.
SPUTANZA kwasasa inahaha kuhakikisha mhezaji Ramadhani Singano anapata haki yake kutokana na kuwepo kwa utata kwenye mkataba wake na klabu yake ya Simba na suala hilo limeonekana kutotatuliwa mpaka sasa licha ya chama hicho kukutana na klabu ya mchezaji huyo (Simba SC) pamoja na TFF.
0 comments:
Post a Comment