Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema litachunguza uhalali wa mikataba miwili ya Simba na winga wake aliyeingia katika malumbano na uongozi, Ramadhani Singano 'Messi'.
Katibu mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema katika mahojiano na moja ya vituo vya redio kuwa watachunguza uhalali wa mikataba hiyo ili kutatua mgogoro uliojitokeza.
"Kikubwa wachezaji lazima wawe makini na mikataba wanayoingia. Tunasikia Simba na Singano wanalumbana, kwa sasa siwezi kusema upande upi una haki maana bado hatajapokea rasmi malalamiko na maelezo kutoka pande zote mbili. Tutachunguza uhalali wa mikataba hiyo," amesema Mwesigwa.
Awali akihojiwa katika kipindi cha 'Sports Bar' cha Clouds TV usiku wa kuamkia leo, Mwesigwa alisema si sawa kuwa na mkataba wenye kipengele kinachoipa mamlaka klabu kuvunja mkataba wa mchezaji muda wowote kwa kumlipa mshahara wa mwezi mmoja.
Wiki iliyopita, Singano alisema hautambui mkataba wa miaka mitatu uliowasilishwa TFF na Simba huku akieleza kuwa mkataba alioingia na mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara ni wa miaka miwili uliokuwa unamalizika Julai Mosi, mwaka huu.
Aidha, katika mkataba mpya wa miaka miwili ambao Simba wamempa ili asaini, kuna kipengele kinachoeleza kuwa klabu (Simba) inaweza kuvunja mkataba muda wowote kwa kumlipa mshahara wa mwezi mmoja, lakini mchezaji (Singano) akitaka kuuvunja, atatakiwa kulipa dola 600,000 (Sh. bilioni 1.2).
"Hii si sawa, hata Kanuni za Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) zinakataza utaratibu huu. Sheria za mfanyakazi pia zinampa faida zaidi mfanyakazi na si kampuni au taasisi katika kuvunja mkataba. Vipi mchezaji alipwe mshahara tu, lakini yeye akiamua kuuvunja alipe dola 600,000? Inapaswa iwe sawa kwa pande zote," alisema Mwesigwa.
0 comments:
Post a Comment