KATIKA moja ya hotuba zake, Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere, aliwahi kusisitiza: "Taifa lolote duniani haliwezi kuendelea bila watu wake kulipa kodi."
Juni 4 mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanga, Uchumi na Biashara kupitia kwa mwenyekiti wake Luhaga Mpina, iliwasilisha taarifa bungeni mjini Dodoma iliyofichua uhujumu mkubwa wa mapato katika sekta ya michezo nchini.
Kamati hiyo ilieleza kuwa serikali haipati mapato ya kutosha kutoka sekta ya michezo nchini, hususan mpira wa miguu ulio chini ya Shirikisho la Soka Tanzaia (TFF) kutokana na uhujumu wa mapato ya milangoni kupitia mfumo dhaifu wa tiketi za kizamani za vishina.
Katika kuhakikisha kadhia hiyo ya uhujumu wa mapato inakomeshwa, kamati hiyo ilitoa tamko la kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuipa sharti TFF kutumia tiketi za kisasa za mfumo wa kielektroniki katika mechi zote za soka nchini.
Agizo hilo lilitekelezwa kwa miezi mitano kuanzia Septemba 2014 kabla ya kupuuzwa siku nne kabla ya mechi ya watani Simba na Yanga iliyomalizika kwa mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara kulala 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 8 mwaka huu.
Aidha, wiki mbili zilizopita TFF iliandaa hafla maalum ya kuadhimisha miaka 50 ya uanachama wake katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda aliyekuwa mgeni rasmi, alisema kuna ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na klabu wakati wa usajili wa wachezaji na makocha.
Mtanda ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga (CCM), alisema pesa wanazolipwa wachezaji wakati wa kusajiliwa hazikatwi kodi na baadhi ya wachezaji wanalipwa mishahara pasipo kukatwa kodi.
Baada ya suala hilo kushikiwa bango na vyombo vya habari, likiwamo gazeti la NIPASHE, TRA ikaiagiza TFF wiki iliyopita kuhakikisha inazibana klabu kulipa kodi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi na TFF kupitia kwa Ofisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Baraka Kizuguto, TRA imeagiza klabu za soka nchini kuhakikisha zinalipa kodi kutokana na kuajiri makocha na wachezaji kutoka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Kamishna wa TRA ameiagiza TFF kupitia kwa katibu mkuu wake: "Klabu zote za soka nchini zinazoajiri walimu, wachezaji kutoka ndani na nje ya nchi wahakikishe wanaweka kipengele cha kodi katika mikataba wanayoingia kuwaajiri."
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa klabu zinapaswa kuwasilisha mikataba yote ya ajira ya wachezaji na walimu wao ili kukokotoa kodi stahiki kwa kila mmoja wao na mikataba yao kugongwa muhuri na stempu.
"Kwa mujibu wa sheria za Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, kifungu namba 7, kila mtu anayepata mapato yatokanayo na ajira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajibika kulipa kodi ya mapato kulingana na kipato chake," ilieleza taarifa hiyo na kuongeza:
"Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Stempu ya mwaka 1973, kifungu namba 5, kila mkataba unatakiwa kugongwa muhuri na stempu na ofisa wa stempu wa TRA."
Hii si mara ya kwanza TRA kutoa tamko la kuikumbusha TFF na klabu kutimiza wajibu wa kikatiba wa kulipa kodi ya nchi, lakini utekelezaji wake unaonekana kutotoa matokeo chanya.
Tafiti mbalimbali zilizofanyika katika sekta ya michezo zinaonyesha kuwa soka ndiyo mchezo unaoongoza kwa kupendwa na watu wengi duniani kote, lakini TRA inaonekana bado haijajipanga kikamilifu kuhakikisha taifa linanufaika ipasavyo na mapato yatokanayo na mchezo huo.
Licha ya kuwapo kwa uhujumu mkubwa wa mapato ya milangoni kupitia tiketi za kizamani za mfumo wa vishina, hesabu za mapato ya TFF zinaonyesha kuwa mapato ya milangoni yanaliingizia shirikisho hilo Sh. bilioni 2.028 ikiwa ni asilimia 29.9 ya mapato yote ya mamlaka hiyo ya juu ya soka nchini kwa mwaka. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati Maalum ya Kudhibiti na Kuboresha Mapato ya TFF iliyotolewa Mei 2011.
Hii ina maana kwamba, mapato ya milangoni yanaweza kuongezeka zaidi ikiwa TRA itatekeleza agizo la Bunge la Juni 4, 2014 kwa kutoa sharti kuitaka TFF itumie tiketi za mfumo wa kisasa wa kielektroniki katika mechi zote za soka nchini.
Ikumbukwe kuwa wakati TRA imetoa tamko la kuibana TFF ili wachezaji na makocha walipe kodi, tayari kuna idadi kubwa ya wachezaji ambao wamesajili kwa makumi na mamia ya milioni ya shilingi hayakukatwa kodi na TRA haijaeleza chochote kuhusu hatua itakazochukua dhidi ya kadhia hiyo.
Nchini Uhispania washambuliaji wa FC Barcolana, Muargentina Lionel Messi na Mbrazil Neymar wana kesi inayowabili kwa kukwepa kulipa kodi na mamlaka zinazohusika nchini humo ziko makini katika kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo haramu.
Katika nchi zilizo makini na zinazotambua umuhimu wa kodi ya wanamichezo, usajili na mishahara ya makocha, wachezaji na watendaji wa klabu za michezo inawekwa wazi kwa umma.
Nchini mwetu tumekuwa nyuma katika ukusanyaji wa kodi katika sekta ya michezo hasa mpira wa miguu. Pesa za usajili na mishahara ya wachezaji na makocha imekuwa ikibaki siri kati ya klabu na waajiriwa, hivyo kurahisisha ukwepaji wa kulipa kodi.
Soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine. Na kwa kutambua umuhimu wa kodi katika kuinua uchumi wa nchi, ninafikiri ipo haja TRA kwa niaba ya serikali kuhakikisha ukwepaji wa kodi unakomeshwa katika soka la Tanzania.
Miradi ya maendeleo, ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya soka hauwezi kufanyika bila wananchi kuwajibika kulipa kodi ya nchi. TFF, klabu, wachezaji, makocha na wadau wengine wa soka wanapaswa kutambua suala hili.
Inashangaza kusikia mamlaka za serikali zinaeleza kuwa mishahara ya wachezaji haikatwi kodi huku baadhi wa wachezaji soka wakilipwa mishahara kwenye viroba katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia.
Nilitarajia kusikia na kuona TRA haiishii kutoa tamko, bali inafuatilia na kusimamia ipasavyo agizo lililotolewa na Bunge la Tanzania kuitaka TFF kutumia mfumo wa kisasa katika kudhibiti hujuma za mapato ya mchezo wa soka. Shirikisho hilo limesajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo linapaswa kutii maagizo ya serikali isipokuwa yanayokwenda kinyume cha kanuni na taratibu za Fifa.
Shime, TRA imeonyesha udhaifu katika kukusanya kodi ya nchi. Ni wakati mwafaka sasa kufuatilia na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo la serikali na sheria ya kodi katika mamlaka ya soka nchini, TFF, klabu na wadau wengine wa shirikisho hilo ili mpira wa miguu usaidie kukuza uchumi wa nchi.
*Imeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.
CHANZO: Gazeti la NIPASHE
0 comments:
Post a Comment