Na Dickson Masanja
Mwezi Mei ambao umemalizika jana, Tanzania tulitia aibu
kwenye anga la michezo haijawahi kutokea, si kwenye soka, ndondi hata kikapu.
Mwezi Mei mwaka huu ulikuwa ni mbaya sana kwa wanamichezo na wapenzi wote wa
michezo kwa kile kilichotokea ndani na nje ya mipaka ya nchini yetu kutokana na
timu zetu kuboronga kwenye michezo.
Tukianza na soka ambao ndio mchezo wenye mashabiki wengi na
unaoongoza kwa kupendwa duniani kote. Mwezi Mei timu yetu ilienda Afrika Kusini
kwa ajili ya kushiriki mashindano ya COSAFA baada ya kupewa mwaliko wa
kushiriki michuano hiyo inayoshirikisha nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Kitu cha kusikitisha ni kwamba, timu yetu ya Taifa ‘Taifa
Stars’ ilipoteza michezo yote mitatu kwenye kundi lake kulikokuwa na timu za
Swaziland, Lesotho, Madagascar na kibonde Tanzania. Kibaya zaidi Stars
haikufunga hata goli moja kwenye michuano hiyo, baada ya kupigwa mechi zote
timu ilirejea nyumbani na sasa inajiandaa kwa ajili ya kufuzu kucheza michuano
ya CHAN pamoja na AFCON.
Wapenzi wa soka walikasirishwa sana na matokeo ya Stars huko
Afrika Kusini na wengine kudiliki kusema kocha afukuzwe akiwa hukohuko ili
akifika hapa achukue kilicho chake na kurejea kwao. Sawa hayo ni maoni na
mitazamo ya mashabiki wa soka na pengingine ni kutokana na machungu ya kufungwa
na timu ambazo zipo chini sana kwenye viwango vya soka vya FIFA.
Lakini swali langu mimi ni je, kufukuza na kuajiri makocha
wapya ni mwarobaini wa tatizo letu? Pasina shaka jibu ni hapana. Basi kama jibu
ni hapana sasa tutafute mwarobaini wa tatizo letu. Tatizo linalotutafuna
Tanzania ni mfumo mzima wa soka letu, kuanzia uongozi, vilabu, wachezaji mpaka
mashabiki.
Kila uongozi mpya uingiapo madarakani huja na sera mpya
pamoja na mipango mipya, bila kuangalia sera na mipango ya uongozi uliopita, uongozi
ulioingia madarakani huanza upya utekelezaji wa sera na mipango yake. Lakini
ikumbukwe inawezekana ilikuwepo mipango mizuri na inayotekelezeka iliyoachwa na
uongozi ulioondoka madarakani, lakini walioingia huitupa kule na kuanza upya.
Badala ya kuendeleza yale mazuri yaliyoachwa wanataka kuanza
upya ili wasionekane kama wanatekeleza sera za waliopita, huo ni ushamba. Nani
kakwambia ukiendeleza kitu kizuri kilichofanywa na mwezio ni vibaya? Hapa ndipo
uongozi wetu huanza kupoteza mwelekeo kwa kutaka kuanza upya kila kitu, wakati
mwingine hata vitu ambavyo si vya lazima.
Jambo lingine ni urafiki, undugu, kujuana na uswahiba kwenye
kazi, viongozi wanapoingia madarakani hutaka kufanya kazi na watu wa karibu yao
bila kuangalia uwezo wa utendaji wa mtu husika. Sikatazi kumuweka rafiki wala
nduguyo kwenye nafasi fulani, kikubwa tuangalie uwezo wake na nafasi anayopewa
kama anaweza kuimudu. Mara nyingi inapotokea ndugu au rafiki wa kiongozi wa
mpira anaonekana dhahiri kushindwa kumudu nafasi yake bado huendelea kubebwa na
kukumbatiwa.
Vilabu vyetu navyo vimekuwa vikiwajaza ujinga baadhi ya
wachezaji, hasa vilabu vyenye nguvu ya kifedha. Hapa namaanisha wachezaji
wanapokuwa kwenye vilabu hivi wanaaminishwa kwamba wao ndio kilakitu ‘lulu’ za
Tanzania, lakini kumbe kuna wachezaji wengine ni wakali kuliko wao na wapo
kwenye vilabu ambavyo havina majina makubwa.
Leo hii Busungu, Mandawa wanapiga magoli zaidi ya 10 lakini
nani anatambua hilo. Kuna wachezaji wangapi wanacheza nafasi moja na wachezaji
hawa kutoka vilabu hivi vyenye nguvu kifedha lanikini hawajafikisha magoli kama
hayo? Lakini wanajiona wao ndio akina Rooney, Ronaldo au Messi kwasababu ndio
wameaminishwa hivyo na klabu zao.
Lakini leo wachezaji kama hawa (Mandawa, Busungu na wengine)
kuitwa kwenye timu ya Taifa mpaka watu wapige debe kama kama wale wapigadebe wa
pale Buguruni-Sheli, hapo utajua ni kwa jinsi gani hivi vilabu vyenye nguvu
vina athiri soka la bongo. Mchezaji anaitwa timu ya Taifa kwasababu yupo timu
fulani na mwingine haitwi kwasababu yupo timu ile.
Ndio maana wachezaji wengi wakifika kwenye vilabu hivyo
wanajiona wamemaliza safari zao za mafanikio na kubweteka, wakati mwingine
hutokea hata wakiletewa ofa kutoka vilabu vya nje wanakataa kwenda wakati
huohuo wakifungwa utasikia wachezaji walikuwa hawajalipwa mishahara. Sasa
unapata wapi ujasiri wa kukataa timu inayokuhitaji wakati hapo ulipo hata
mshahara wa mwezi unalipwa kwa manati?
Tuachane na hao twende kwa wachezaji wenyewe, kiukweli
malengo ni kitu kizuri sana maishani. Kuma unaishi halafu huna malengo ni bora
ungeendelea kubaki mtoto miaka yote. Kwenye malengo kuna malengo ya muda mfupi
na yale ya muda mrefu, kama leo ukiniuliza nimefikia wapi kuhusu malengo yangu
niliyojiwekea naweza kukupangia yale yaliyotimia na ambayo hayajaimia kwasababu
nina malengo.
Wachezaji wa bongo sasa, wanacheza soka ili mradi maisha
yanaenda. Hawana malengo kabisa, wanafurahia kuonekana live kwenye TV ili wawe
maarufu basi miaka isonge mbele. Au wengingine malengo yao ni kucheza kwenye
hivi vilabu vyetu vikongwe basi. Sina maana mbaya hapa ila wengi wanapofika
hapo ndo wale niliokwambia wanaanza kujiona akina Rooney, Ronaldo au Messi na
hii ni kutokana na kutokuwa na malengo.
Mfano mzuri hapa ni Mbwana Samatta, huyu jamaa anaonekana
anajitambua na uwezo wa soka anaounesha uwanjani ni sawa na uwezo wa akili yake
kichwani. Sitaki kukwambia Samatta ametokea wapi mpaka sasa hivi anacheza TP
Mazembe, jiulize mwenyewe amekaa kwa muda gani pale Msimbazi na akaonekana
anajua akanyakuliwa. Huyu jamaa anamalengo ndiyo maana hata pale Mazembe anaona
bado hajafika hivyo anajituma zaidi ili asonge mbele zaidi kutimiza malengo
yake.
Samatta amewakuta wachezaji wangapi pale Simba na akaondoka
akawaacha? Anamalengo ndio maana anapota nafasi aitumia kwa kujituma ili siku
moja ndoto zake na malengo aliyojiwekea yatimie.
Sasa hawa wachezaji wasiojielewa na wasio na malengo
wanaathiri vipi timu ya Taifa, kwanza kucheza kwenye hivyo vilabu vyenye nguvu
kunawapa kiburi wajione wao ni ‘mafaza’ kitu kinachowafanya wasijitume kuanzia
kwenye mazoezi mpaka kwenye mechi. Kitu kingine wanajua kabisa ‘piga ua
garagaza’ lazima niitwe kwenye timu ya Taifa na lazima nicheze tena kikosi cha
kwanza.
Mchezaji kujiona yeye yupo juu ya timu ni kuliua soka letu,
kila mchezaji anapaswa kujua umuhimu na wajibu wake kwenye timu ya Taifa,
unapopewa nafasi ya kucheza kwenye timu ya Taifa hebu tushawishi tuone ni kwa
kiasi gani unastahili kutuwakisha sisi kwenye timu yetu maana ndiyo timu pekee
inayotuweka kwenye jukwaa moja.
Sasa kwa hali hiyo unataka tubadishe kocha, sawa tutamleta
mwingine nay eye akivurunda tunamleta mwingine halafu mwisho wa siku inakuwaje?
Hivi kwani tangu tumeanza kuajiri makocha wa kigeni ni kocha gani ambaye
ametupa mafanikio zaidi ya Arcio Maximo kuipeleka Tanzania kwenye mivhuano ya CHAN,
tukamfukuza wakaja wengine na tunaendelea kuwafukuza.
Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu, kauli hii aliitoa Rais
wa awamu ya pili mzee Ally Hassan Mwinyi akimaanisha hata wale watu wasiojua
kunyoa ndio sehemu wanayojifunia kunyoa.
Sasa kwa hayo niliyoyaoodhesha hapo juu tutaendelea kunyolewa tu.
Kwenye makala ijayo, nitakuletea mwendelezo wa aibu nyingine
kwenye michezo iliyotokea mwezi Mei, hii itakuwa ni kwenye mpira wa kikapu na
masumbwi.
0 comments:
Post a Comment