Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, amesema ana imani akicheza sambamba na mwenzake Malimi Busungu, watakuwa na nafasi kubwa ya kufunga mabao mengi kikosini.
Katika mazoezi ya Yanga juzi Ijumaa, Tambwe alifunga mabao matatu na Busungu aliyesajiliwa kutoka JKT Mgambo naye akafunga matatu, huku jambo la kufurahisha likiwa ni wachezaji hao kupeana pasi za mabao waliyofunga.
Yaani ipo hivi, mabao yote aliyofunga Tambwe amepokea pasi za mwisho za Busungu na yale aliyofunga Busungu ni ya pasi za mwisho za Tambwe.
Hata hivyo, Tambwe alisema: “Huyu Busungu ni mzuri sana na nikiendelea kucheza naye hivi, tutakuwa tunafunga tunavyotaka, lakini natakiwa kuthibitisha ubora wake kama nikicheza naye katika mechi kama tatu hivi.”
Tambwe amesema anajua ni mapema kuzungumzia kombinesheni yake na uwezo wa Busungu kwa muda mfupi aliofanya naye mazoezi lakini baada ya mechi tatu atakuwa na jibu kamili.
Tambwe alisema: “Huyu jamaa siyo mbaya kwani anatoa pasi zenye macho, anamiliki mpira vizuri, ana nguvu ya kupiga mashuti ndani na nje ya eneo la hatari, unadhani huyo akitulia hali itakuwaje?”
“Simsifii kwa kuwa nacheza naye kikosi kimoja lakini hata mashabiki wameona uwezo wake na kama akiendelea kujituma namna hii, Yanga itafaidika naye sana.”
0 comments:
Post a Comment