MSHAMBULIAJI wa kimataifa
wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Zesco United ya Zambia,
Juma Liuzio Ndanda amesema timu nyingi za nchi hiyo zinamiliki viwanja binafsi
na zinajali sana maslahi ya wachezaji tofauti na Tanzania.
Akizungumza na MPENJA BLOG kutoka Zambia, Liuzio
ameongeza kuwa timu za Zambia zina udhamini wa mashirika mbalimbali yanayosababisha ushindani kuwa mkubwa zaidi.
“Utofauti wa Tanzania na
Zambia ni mkubwa, kwanza ukiangalia timu
nyingi huku zinamiliki viwanja vyao binafsi na vizuri. Pia timu nyingi zinadhaminiwa
na mashirika mbalimbali, kwahiyo vitu vingi vinakuwa rahisi kwao na ndio maana ushindani
ni mkubwa tofauti na Bongo ambako kuna timu chache sana zenye ushindani”.
Amesema Liuzio, mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar.
Aidha, Straika huyo ambaye
pia hujumuishwa mara kadhaa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa
Stars, amefafanua kwamba viongozi wa Zambia wanajitahidi sana kufuata uweledi
wa kazi.
“ Kwa upande wa uongozi, kila kiongozi
anacheza part yake ya kazi, huwezi
kusikia manager wa timu anampangia kocha kikosi na wanajali sana wachezaji wao hususani
maslahi ya mchezaji binafsi”. Ameongeza Liuzio.
Kutokana na ushindani
uliopo katika kikosi cha Zesco kilichojaa wachezaji wazawa na watano tu wa
kigeni, Liuzio amesema jitihada binafsi ndizo zinamfanya apate namba kwenye
kikosi cha kwanza kwa muda wote.
“Mimi kikubwa huwa nafanya
mazoezi yangu binafsi tofauti na ya timu, so muda mwingi nakuwa fit na pia napenda sana
kumsikiliza kocha, nafanya vile
anavyoelekeza kwa jitihada zaidi”.
Luizio alianza kucheza soka
katika timu ya Docks ya Morogoro , mwaka 2011 alichaguliwa timu ya mkoa wa Morogoro
iliyoshiriki michuano ya Taifa Cup na
ndipo akasajiliwa na Polisi Moro ambapo alicheza ligi daraja la kwanza na
kufanikiwa kupanda nayo ligi kuu, lakini akaachwa.
Baada ya hapo akasajiliwa
na Mtibwa Sugar B mwaka 2012, lakini kutokana na kuonesha kiwango cha juu
alipandishwa timu A ambapo alicheza ligi kuu Tanzania bara na baadaye
kusajiliwa na Zesco.
0 comments:
Post a Comment