WEKUNDU wa Msimba Simba
wanajiandaa kumchukulia hatua za kisheria mshambuliaji wao mahiri, Ramadhani
Singano ‘Messi’ kwa kuituhumu klabu hiyo kughushi mkataba wake.
Afisa habari wa Simba, Hajji
Manara amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu, Msimbazi,
Kariakoo, Dar es salaam kwamba , Simba haijaghushi mkataba wa Singano kama
anavyodai yeye na meneja wake Hamis Ramadhan ambaye ni kaka yake wa damu,
lakini kwasasa ndiye msimamizi wake.
“Simba inatambua mkataba wa
Messi unamalizika mwakani na si mwaka huu kama anavyodai. Kama kuna klabu
inamuhitaji mchezaji huyo, bora ijitokeze na kufanya mazungumzo ramsi na Simba,”amesema
Manara na kusisitiza: “Kitendo
alichokifanya Messi kinafanyiwa kazi na mamlaka za ndani za Simba na baadaye
tutatoa tamko la hatua tuliyochukua,”.
Siku za karibuni, Singano
ameishutumu klabu yake kwa kughushi mkataba wake akidai kuwa mkataba wake
halali ni wa miaka miwili aliosaini Mei mosi mwaka 2013 na unatakiwa kumalizika
Julai 1 mwaka huu.
Simba wao wana mkataba wa
miaka mitatu uliosainiwa mei 1, 2013 na utamalizika Julai 1, 2016.
Wakati hayo yakiendelea
tayari Simba walishatengeneza mkataba mwingine wa Messi uliotakiwa kusainiwa
juni 1 mwaka huu, lakini nyota huyo aligoma akishinikiza kwanza tatizo la
mkataba wake wa kwanza lipatiwe ufumbuzi, halafu mkataba mpya urekebishwe
baadhi ya vipengele.
Hata katika mkataba wa
kwanza, Messi anadai kuna vipengele havijatimizwa mathalani kulipiwa kodi ya
nyumba.
0 comments:
Post a Comment