Mwalimu aliyemfundisha Singano, Abuu Rashid Laizer
SIKU mbili baada ya Simba kudai imemsomesha mshambuliaji
wake, Ramadhan Singano ‘Messi’, walimu wa shule aliyosoma ya Al-Farouq Islamic
Seminary wameibuka na kukanusha madai hayo.
Mtandao huu umefika shuleni hapo na kukutana na mwalimu wa
Singano, Abuu Rashid Laizer anayefundisha masomo ya Historia na Geografia
pamoja na mlezi wake Hashimu Omary Poli.
Shule aliyosoma Singano
Mwalimu Laizer katika maelezo yake amesema: “Ramadhan Singano
amelelewa hapa kuanzia darasa la pili mpaka anamaliza kidato cha nne mwaka 2010”.
“Hapa alikuwa analelewa katika idara zote, tukiwa na maana
katika malezi yake kama kijana, kielimu na mambo mengine yanayomuhusu. kwanza
ni mtoto yatima, hana baba wala mama”.
“Shirika la Africa Muslim Agency lilichukua jukumu kutoka
kwa ndugu zake kwa lengo la kumuwezesha kupata elimu. kama mnavyojua,
unapomsaidia yatima kuna mafanikio ambayo mwenyezi Mungu atakuwezesha mbele ya
safari. Moja ya sera ya shirika ni kusaidia yatima, Ramadhan ni miongoni mwao”
“Kuna vitu vingine watu wanazungumza labda kutokana na
maslahi yao na wanajaribu kupotosha umma, lakini kiuhalisia huyu bwana (Singano)
alikuwa hapa na patroni wake yupo”.
“Alikuwa anatokaje hapa mpaka alipoonana na Simba? Wengi
wanadhani alitoka Simba B, lakini Simba walimuona akicheza shuleni kupitia kwa
kocha wake aliyekuwa akiitwa kibonge na aliondoka mwaka 2007 wakati sisi
tunaingia. Licha ya kuondoka, kibonge
bado alikuwa na ushirikiano na kijana wetu pamoja na kaka yake Ramadhan Hamis”.
“Kuna vitu vingine inabidi tuseme ili tusionekane kumbeba
mtu fulani. Mwaka 2007 nikiwa mwalimu wa michezo nikimsaidia mwalimu anayeitwa
Saleh Haruna, nilikuwa nahusika kutoa vibali kwa Singano kwenda kukutana na wachezaji
wenzake wa Simba B”
“Ni muda mrefu, lakini imekuja kuonekana hivi juzi kuwa Singano
ni moja ya wachezaji wanaoweza kuisaidia Simba.
Kuanzia 2009 mpaka 2011 timu kubwa iliona anaweza kufaa, lakini yeye ni
yatima na wakati anasoma kila kitu kuanzia kula, kulala mpaka madaftari viligharamiwa
na shirika”
“Vitu vyote walikuwa wanapewa na shirika pindi wakifungua
shule. Hakuna mtu aliyekuwa akimlipia ada, mimi sijaona, labda kama mtu anazo
risiti alizokuwa anamlipia alete tuzione na kuthibitisha”.
“ Utaratibu wetu wa ada ya watoto yatima huwa inakatwa moja
kwa moja Damam, Quwait, ambako ni makao makuu ya Idara ya elimu ya ‘Africa Muslim
Agency’ duniani, lakini kwa Tanzania kuna tawi lake hapa Dar es salaam na Sheikh Kassim Mzee
ndiye aliwatafuta akina Singano na wenzake”.
Baada ya kuzungumza na mwalimu, tukapata fursa ya kuonana na
mlezi wa watoto yatima shuleni hapo, Hashimu Omary Poli ambaye amefanya kazi
toka mwaka 1997 mpaka leo.
Katika malezo yake Poli amefafanuwa kuwa:
“Ramadhan Singano nilimpokea toka mwaka 2001 akiwa darasa la
nne. Amesoma hapa mpaka alipomaliza kidato cha nne chini ya udhamini wa shirika
la Africa Muslim Agency”.
“Kijana huyu toka alipokuwa mdogo kipaji chake kilidhihirika
kwenye suala la michezo, alionesha uwezo mkubwa na kwa bahati nzuri kulikuwa na
mwalimu Kibonge aliyekuwa karibu nao sana.
Mwalimu huyu alipewa fursa kubwa sana ya kuwa nao na kukuza vipaji vyao”.
“Nashukuru Mwenyezi Mungu mpaka anafika ‘fomu foo’ alikuwa
kijana anayependa sana mpira na akapata bahati ya kujiunga na Simba. Tukawa
tunamsikia Ramadhani Yahya Singano ni mchezaji na alikuwa anakuja kuwasalimia
wenzake na wakati mwingine anawaletea misaada”.
“Tunashukuru kwamba anakumbuka fadhila za Maustadh wake,
anakumbuka jinsi alivyolelewa, aliishi na wenzake vizuri, tunamuombea kila la kheri”.
“Ninachokifahamu mimi kama mlezi nilimpokea akiwa mdogo.
Suala zima la kimalezi, udhamini wa kusomeshwa shule ilikuwa chini ya Shirika
la Africa Muslim Agency. Wao ndio waliomdhamini na walimpokea akiwa mdogo kama
wanavyowapokea watoto wengine yatima”. Amesema Poli.
Baadhi ya nyaraka za Singano katika shule aliyosoma
Mwanzoni mwa wiki hii Msemaji wa Simba, Hajji Sunday Manara
alisema klabu hiyo imegharamia masomo ya Singano na wanashangaa kijana wao
kukosa fadhila.
Manara alisema: “Hivi
mnajua Messi tumemtoa wapi Simba? Unajua Ramadhan Singano amesomeshwa na klabu
ya Simba? Mnafahamu hilo? Kasomeshwa IT
na klabu ya Simba, Mnajua fadhila ambayo
klabu ya Simba imemfanyia?”
“Hao wanaosema wazazi wake walikuwa wapi wakati klabu ya
Simba inamsomesha? Nauliza, walikuwa wapi? Klabu ya Simba imegharimia haya.
Ninyi waandishi ndio mnaandika vilabu havithamini wachezaji chipukizi. Sisi ndio
klabu pekee yenye wachezaji zaidi ya asilimia 75 tuliowatoa kwenye mpango wetu
wa soka la vijana. Hawa tunawakuza na bado tunawapa ofa ya usajili”
Singano ameingia kwenye mgogoro na klabu yake akidai
imeghushi mkataba wake.
Simba ina mkataba wa miaka mitatu uliosainiwa mei 1, 2013 na
unatakiwa kumalizika julai 1, 2016, wakati Singano ana nakala ya mkataba wa
miaka miwili aliosaini mei 1, 2013 na unamalizika julai 1, 2015.
Nakala ya mkataba wa miaka mitatu waliyonayo Simba pia ipo TFF,
lakini Singano anadai hakusaini mkataba huo na anautambua wa miaka miwili.
Licha ya suala hilo la mkataba, bado Singano
hajatimiziwa baadhi ya stahiki zake katika mkataba wake miaka miwili ikiwemo
suala la kodi ya nyumba.
Muonekano wa shule aliyosoma Messi
0 comments:
Post a Comment