Siku chache baada ya kutemwa katika usajili Yanga, Lansana Kamara jana asubuhi mapema aliibuka katika mazoezi ya SC Villa ya Uganda na leo anataichezea timu hiyo dhidi ya Yanga kwenye mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa.
Juzi Jumatano Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm bila kuficha alimuambia Kamara raia wa Sierra Leone, hana nafasi ya kusajiliwa katika kikosi chake kwa kuwa ana uwezo wa kawaida.
Baada ya kuelezwa hayo, Kamara akiwa na wakala wake Gibby Kalule wakatimua zao na jana asubuhi walitinga katika mazoezi ya Villa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ubungo Plaza.
Kocha wa Villa, Ibrahim Tillya amesema: “Huyu mchezaji amekuja hapa katika mazoezi na tutamtumia kesho (leo) katika mechi yetu na Yanga na akifanya vizuri tutamsajili.”
Hata hivyo Kamara hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusu kuonekana kwake katika mazoezi hayo akiwa sambamba na wakala wake.
Yanga leo jijini Dar es Salaam inacheza na Villa katika mechi ya kirafiki ya kuchangia fedha za ujenzi wa makazi watoto waishio katika mazingira magumu na kuwachangia watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albinism’.
0 comments:
Post a Comment